
MWANANCHI
Mali za Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba zimetangazwa kupigwa mnada kutokana na kushindwa kulipa deni analodaiwa na Benki ya CRDB.
Mali hizo zinahusisha eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 2,214
lililopo Mbezi Tangi Bovu, Dar es Salaam, kiwanja namba 1030
kilichosajiliwa kwa jina la John Damiano Komba na Salome Komba.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwenye vyombo vya habari, Kampuni ya Uwakili ya Mpoki & Associates Advocates
inayoiwakilisha CRDB imetangaza kuuza eneo hilo la kibiashara
lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mafuta, maduka makubwa,
benki, sehemu ya kufanyia mazoezi, hospitali na huduma nyingine za
kijamii.
“Tayari
eneo hilo lina nyumba kubwa ya kuishi upande unaotazamana na barabara
mpya ya Bagamoyo. Kwa upande wa kusini mwa jengo kuu linalotazama
barabara hiyo kuna nyumba nyingine ya kuishi, fremu za maduka na ofisi,” ilisomeka sehemu ya tangazo hilo.
Alipoulizwa juu ya gharama halisi anazodaiwa Kapteni Komba na muda wa deni hilo, mmiliki wa Kampuni ya Mpoki & Associates Advocates inayoratibu mnada huo, Mpale Mpoki alisema maelezo yote yanayohusu kiasi cha mkopo na muda wa deni yatajibiwa na CRDB wenyewe.
MWANANCHI
Baada ya subira ya wiki mbili ili wenyeviti na wajumbe Mtaa wa
Migombani – Segerea, Dar es Salaam waapishwe na mamlaka husika bila
mafanikio, wananchi wameamua kuwaapisha viongozi hao kwa kutumia wakili
binafsi.
Wakati hali hiyo ikitokea Dar es Salaam, wilayani Rombo mkoani
Kilimanjaro baadhi ya wenyeviti wa vijiji walioshindwa wamekataa
kuwaachia ofisi viongozi wapya wakidai kuwa ofisi hizo ni mali ya CCM.
Katika tukio la Segerea lilitokea jana asubuhi Segerea Mwisho, Japhet Kembo aliapishwa kuwa ‘mwenyekiti’ pamoja na ‘wajumbe’ watatu ambao ni Rose Bernard Mhagama, Nyangeto Justin na Ramadhan Seif wote wa Chadema bila kuishirikisha Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Kembo alisema wananchi wamechoshwa na danadana wanazopigwa na Manispaa ya Ilala za kutowaapisha viongozi waliowachagua.
“Wananchi wamemtafuta wakili ambaye amekuja kusimamia suala hili kisheria na ndiyo maana zoezi limefanywa hadharani,”– Kembo.
Kembo alisema katika nafasi ya uenyekiti alipata kura 547, Uyeka Idd wa CCM kura 273 na Erick Mchata wa NCCR-Mageuzi kura 205.
MWANANCHI
Wakati Taifa zima likiwa katika
kitendawili cha kumjua kiongozi wa nchi atakayepatikana baada ya
Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Rais ajaye anafahamika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu jana, Jaji Warioba
alisema si kazi ngumu kwa Watanzania kumfahamu rais ajaye kwa kuwa
katika miaka 50 tangu tupate uhuru, Watanzania wanazijua sifa za
kiongozi bora.
“Tatizo
la kumjua rais afaaye tunalikwepa lakini linafahamika. Wanaotumia fedha
na lugha chafu katika kampeni na hao ndiyo wasiotakiwa”– Jaji Warioba.
Hadi sasa wanasiasa zaidi ya 20 wakiwamo
wa CCM na upinzani wamekuwa ama wanatajwa au wameonyesha nia ya
kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Ukiacha wale wanaotajwa, wanasiasa waliotangaza nia hiyo kutoka CCM ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed akitangaza nia kupitia ADC.
Kuhusu tetesi za kuwania urais Jaji Warioba alisema amelitumikia Taifa kwa muda mrefu na aling’atuka kwa mapenzi yake, hivyo hawezi kurudi tena katika siasa.
NIPASHE
Misamaha ya kodi imeongezeka kutoka Sh.
trilioni 1.48 mwaka 2012/13 hadi Sh. trilioni 1.82 ikiwa ni ongezeko la
Sh. bilioni 334, kwa mwaka 2013/14.
Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema hali hiyo inashangaza kwa kuwa
kamati hiyo inapiga kelele misamaha hiyo kupungua, lakini inazidi
kuongezeka jambo ambalo linaonekana ni wapiga porojo.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe
alisema wakati kamati hiyo ikihojiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), juu ya hoja mbalimbali za kamati zilizotakiwa kutolewa maelezo
katika kikao kilichopita.
Kamishna wa TRA, Richard Beda, alisema
ongezeko hilo linatokana na miradi mikubwa ya barabara na madaraja
pamoja na ujenzi wa bomba la gesi na miradi mbalimbali ya mafuta na
gesi.
“Misamaha hii imejikita katika kodi
ya ongezeko la thamani (VAT), (Special Relief au misamaha maalum) kwa
kampuni zinazohusika na ujenzi na utafutaji na ujenzi wa bomba la gesi,
kwa daraja la Kigamboni pekee kuna msamaha wa Sh. bilioni 676, na mafuta
na gesi ni Sh. bilioni 100… sheria mpya ya VAT ndiyo itapunguza
misamaha hii, tunataka iharakishwe,”– Zitto Kabwe.
Zitto
alisema kampuni binafsi zinapata misamaha ya Sh. bilioni 340 huku
msamaha wa VAT ikiwa ni Sh. bilioni 639 na kwamba lengo la kamati ni
kuona misamaha hiyo inafikia chini ya asilimia moja ya pato la taifa.
NIPASHE
Mashine ya mionzi ya kutolea huduma ya matibabu ya saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini
Dar es Salaam, inatarajia kuanza kufungwa wiki hii ikiwa ni sehemu ya
ukarabati wake hivyo kuendelea kukabiliana na ukosefu mitambo hiyo
katika hospitali nyingi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid alisema
mashine hiyo ni moja ya zilizoharibika na kwamba ufungaji wake unaanza
ndani ya wiki hii baada ya wataalamu na vifaa vyake kutarajia kuwasili
kutoka Canada.
Aliongeza kuwa serikali pia ipo katika
mkakati wa kuleta mtambo mwingine mpya wa mionzi ambao utagharimu Dola
za Marekani milioni moja.
Kwa mujibu wa Dk. Rashid, gharama hizo zitachangiwa na Serikali kwa asilimia 50 na asilimia 50 zitatolewa na Shirika la Kimataifa la Atomi ‘International Atomic Agency.’
Kuhusu hali ya saratani nchini, alisema,
hali bado ni mbaya kwani hadi sasa idadi ya wagonjwa inaendelea
kuongezeka na hadi sasa kuna wagonjwa 33, 834 ambao wanaugua ugonjwa huo
nchini kote.
Kati ya idadi hiyo, 7, 304 wanasumbuliwa
na saratani ya shingo ya kizazi na iliyobaki ni kwa aina nyingine
ikiwamo ya ngozi na matiti na chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya
kizazi imeanza kutolewa katika mkoa ya Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Waziri Rashid, walengwa wakubwa wa chanjo hiyo ni pamoja na wasichana kwani katika umri huo kuna uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huo.
MTANZANIA
Wakati Watanzania wakisubiri kujua
hatima ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
aliyewekwa kiporo na Rais Jakaya Kikwete baada ya kuhusishwa na kashfa
ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow,
Waziri huyo amesafiri kwenda Davos nchini Uswisi kuungana na rais katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani maarufu kama ‘World Economic Forum’.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Muhongo ameondoka nchini jana.
“Profesa
ameondoka leo (jana) kwenda Switzerland (Uswisi) ambako ataungana na
rais kwenye mkutano huo utakaoanza Januari 21 hadi 24,” kilipasha chanzo hicho.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu, ili kuthibitisha taarifa hiyo, hakuweza kutoa jibu.
Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam Desemba 22 mwaka jana, Rais Kikwete alitangaza kumuweka kiporo Profesa Muhongo
akisubiri kupata ufafanuzi kuhusu mambo kadha wa kadha ili kujiridhisha
kabla kuujulisha umma juu ya hatua atakazochukua dhidi ya waziri huyo.
MTANZANIA
Vurugu zimetokea jana kwenye ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini baada ya makundi yanayopingana ndani
ya Chama cha ACT-Tanzania kukutana ana kwa ana katika ofisi hiyo kwa
ajili ya kikao cha usuluhishi.
Baada ya kukutana kwa makundi hayo, ghafla walitokea vijana wanaodaiwa kukodiwa na Mwenyekiti aliyesimamishwa, Kidawi Limbu na kumvamia Katibu Mkuu wa muda wa chama hicho, Samson Mwigamba.
Vurugu hizo zimetokea ikiwa ni siku
chache baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho kumsimamisha uongozi
Limbu na kumwondoa katika nafasi yake aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Leopold Mahona kwa makosa ya kinidhamu.
Mwigamba alidai vijana hao wamekodiwa na Limbu kwa lengo la kumfanyia vurugu baada ya kuona mikakati yake imekwama ndani ya chama.
“Limbu alikuja na kundi la vijana kama 12, kati yao wawili aliwasafirisha kwa ndege kutoka Arusha na mmoja anaitwa Gerald Emmanuel, pia alikuwamo Mwenyekiti wa Geita, Katibu Uenezi Ukonga, Katibu Uenezi Jimbo la Kinondoni pamoja na kina Mahona.
“Wakati tunatoka kikaoni nikawa
pale nje nasubiri gari linichukue, akaja Gerald huku akishika shati
langu akidai ananidai shilingi milioni moja na lazima nimlipe pale pale,
nilishangaa sana na hapo ndiyo nikajua kuna kitu Limbu amefanya ili
wale vijana wanivuruge na baadaye nikasirike na kuonekana nimepigana”– Mwigamba.“Limbu alikuja na kundi la vijana kama 12, kati yao wawili aliwasafirisha kwa ndege kutoka Arusha na mmoja anaitwa Gerald Emmanuel, pia alikuwamo Mwenyekiti wa Geita, Katibu Uenezi Ukonga, Katibu Uenezi Jimbo la Kinondoni pamoja na kina Mahona.
MTANZANIA
Mtoto wa miaka 15 mkazi wa Manzese jijini Dar es salaam, anadaiwa kubakwa na kulawitiwa na mjomba wake aliyetajwa kwa jina la Hassan Maumba ambaye
kwa sasa anashikiliwa na polisi katika kituo cha Urafiki ambaye alikuwa
akifanya kitendo hicho kwa muda wa miaka mitatu huku akitishia kuua.
Mbali na kulawitiwa mtoto huyo pia
alidaiwa kulazimishwa na mjomba wake huyo kumnyonya damu baada ya
kujikata na wembe, huku akimtishia na kisu kama angekataa au kutoa
taarifa hizo kwa mtu yoyote.
Mtoto huyo ambaye ni yatima alimaliza
darasa la saba mwaka jana na alisema mjomba wake alianza kumfanyia hivyo
wakati akienda bafuni kuoga.
“Siku
ya kwanza nilipoingia bafuni, mjomba alikuja na kuanza kuniingiza vidole
sehemu za siri huku akinitisha nisimwambie mtu,aliendelea hivyo na
kufikia hatua ya kuniingilia kinyume na maumbile huku mke wake akiwa
hajui na kunitishia kuniua kama ningesema“alisema mtoto huyo huku akitokwa machozi.
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment