BAADHI ya wanasiasa wa muungano wa
Jubilee sasa wanaonya kuwa watafunga viwanja vya ndege nchini kumzuia
Rais Uhuru Kenyatta kutii amri ya mahakama ya ICC ya kumtaka ahudhurie
kikao cha kesi yake mapema mwezi ujao.
Hayo yalijiri
huku mrengo wa Jubilee ukitazamiwa kuandaa mkutano wa dharura Jumanne
kujadili ikiwa Rais Kenyatta atatii mwito huo au ataupuuza.
Wakiongozwa
na mbunge wa Dagoretti Kusini Bw Dennis Kariuki Waweru (TNA), walisema
hakuna vile mahakama hiyo inaweza kuhujumu uhuru wa taifa la Kenya kwa
kumshurutisha Rais ahudhurie kikao cha kumshtaki.
“Hiyo ni sawa
na kutunyang’anya bendera yetu ambayo ndiyo ishara ya uhuru wetu na
kuipeleka katika taifa la kigeni na kuipandisha huko kana kwamba sisi ni
waathiriwa wa kikoloni,” akasema.
Alisema ikiwa
wazo lake litatiliwa maanani na mrengo wa Jubilee, basi wanasiasa wote
wa mrengo huo wanafaa kujipeleka katika mahakama hiyo kumwakilisha Rais,
huku Wakenya wanaomuunga mkono wakifunga viwanja hivyo.
Walishikilia
kuwa hatua hiyo ya kumtaka Rais ajiwasilishe katika mahakama hiyo mnamo
Oktoba nane mwaka huu ina njama fiche ya kisiasa na hainuii uwezekano wa
haki kuhusu kesi yake ila inataka kumuaibisha.
Rais Kenyatta
na Naibu wake Bw William Ruto na pia mtangazaji Joshua arap Sang’
wanajitetea katika mahakama hiyo kufuatia kudaiwa kuwa walihusika na
ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.
Katika ghasia hizo, takriban watu 1, 500 waliaga dunia huku maelfu wakifurushwa makwao na kugeuzwa kuwa wakimbizi wa ndani.
Kiongozi wa
walio wengi katika seneti Bw Kithure Kindiki akiongea katika hafla ya
Naibu Rais katika Shule ya Sekondari ya Tumutumu Kaunti ya Nyeri alisema
kuwa mahakama hiyo haina haki ya kumwagiza Rais ajiwasilishe binafsi.
“Yeye
hataulizwa maswali yoyote na mahakama hiyo kwa kuwa hakuna ushahidi
uliowasilishwa na nia kuu ya kiongozi wa Mashtaka Bi Fatou Bensouda ni
kumuabisha mbale ya runinga za ulimwengu,” akasema.
Aidha,
alisema kuwa kufikia sasa kesi dhidi ya Rais imesambaratika na kile Bi
Bensouda anafuatilia ni kucheza siasa za mataifa ambayo hayamtakii Rais
Kenyatta nia njema katika mamlaka yake.
Alisema kuwa
kwa sasa mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw Githu Muigai amedhihirishia
mahakama hiyo kuwa inakiuka haki za mshukiwa kwa kumtaka atoe habari za
kujihukumu, hii ikiwa ni kinyume na utaratibu wa haki katika kesi yoyote
ile.
Habari muhimu
Tayari, Bi
Bensouda ameomba mahakama hiyo imshinikize Rais Kenyatta ashirikiane na
mahakama hiyo kutoa habari muhimu kuhusu akaunti zake za benki, mali
anayomiliki hapa nchini na pia habari za ujasusi kumhusu katika kipindi
cha kabla na cha wakati ghasia hizo zilikuwa zinaendelea.
Wengine ambao
walinga mkono msimamo huo ni Bw James Mwangi Gakuya (TNA) ambaye ni
mbunge wa Embakasi Kaskazini aliyesema kuwa taifa la Kenya haliwezi
kugeuzwa kuwa kisiwa ndani ya Uholanzi kupitia hujuma za mamalaka ya
Rais wa taifa huru.
Wiki jana,
wanasiasa wengine wa Jubilee walisema kuwa kesi dhidi ya Rais katika
Mahakama hiyo ina njama ya kumtatiza katika uchaguzi mkuu ujao wa 2017.
Wanashikilia
kuwa kesi hiyo haina msingi wowote, bali iliandaliwa kwa misingi ya
kisiasa ambapo mataifa kadha hayakumtaka agombee urais katika uchaguzi
wa 2013.
Kwa hivyo,
walimtaka Bi Bensouda atupilie mbali kesi hiyo wakisema kuwa kufikia
sasa ameonyesha wazi kuwa hana ushahidi wowote
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment