KULIZUKA vurumai katika shule ya msingi
mwanamume alipomiminiwa risasi na kuuawa papo hapo kwa kujaribu
kumshambulia Mbunge wa Ndia Stephen Ngare.
Wakati wa
kisa hicho cha kushangaza, mlinzi wa mbunge huyo,Bw Joseph Mushumba, na
mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Ndando, Bw Sammy Mwangi, walijeruhiwa
vibaya.
Bw Ngare alikuwa ametembelea sehemu hiyo kukagua miradi ya maendeleo.
Waathiriwa hao walikatakatwa mara kadha kwa upanga na mvamiaji huyo huku wakimkinga Mbunge huyo ambaye alikuwa analengwa.
Walioandamana na Mbunge huyo, wanafunzi na wazazi walitorokea usalama wao huku milio ya risasi ikitamba hewani.
Pia
waliotorokea usalama wao ni maafisa wawili wa polisi waliovalia sare
rasmi lakini hawakuwa na silaha zozote. Jukumu la kumkinga Mbunge huyo
liliachiwa mwalimu huyo mkuu pamoja na mlinzi wake.
Fujo hilo zilivuruga shughuli za masomo shuleni humo mchana kutwa.
Mbunge huyo alianza ziara yake majira ya saa nne asubuhi akiandamana na maafisa wa Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (CDF).
Baada ya
kuwasili Ngando, alilakiwa kwa shangwe na wazazi, walimu na wazazi.
Alipokuwa akielekea katika madarasa mapya yaliyofadhiliwa na hazina
hiyo, mwanamume mmoja alichomoka kutoka kwa umati na kumkabili mbunge
huyo.
Alimlenga
mbunge huyo tayari kumkata kwa upanga huo lakini mwalimu mkuu akamzuia.
Bw Mwangi alijikakamua kumsitiri mbunge huyo lakini akazidiwa nguvu na
mvamizi huyo anayetoka lokesheni ndogo ya Thigirichi.
Ni wakati huo
ambapo alimkatakata Bw Mwangi mara kadha kichwani kabla ya kumwangusha
chini. Ni wakati huo ambapo mlinzi wake alijaribu kumkabili mwanamume
huyo lakini naye akakatwa kwenye mkono wake wa kushoto.
Huku
akibubujikwa damu, mlinzi huyo alichomoa bastola yake na kummiminia mtu
huyo risasi, hali iliyowafanya wakazi hao kutoroka kwa hofu.
Mhasiriwa
huyo alianguka chini huku Mbunge huyo na mlinzi wake wakiingia kwenye
gari lake na kufululiza hadi kituo cha polisi cha Sagana.
Baadaye,
waathiriwa walipelekwa katika kituo cha afya cha Saganga kisha
wakahamishwa hadi hospitali ya Jamii mjini Karatina baada ya hali yao
kudhoofika.
Mwalimu huyo mkuu alijeruhiwa mara kadha na akapelekwa hospitalini akiwa amezimia.
Mshtuko
Haikubainika mara moja ni kwa nini mvamizi huyo alitaka kumdhuru Mbunge lakini wafuasi wake walishuku alichochewa kisiasa.
Bw Ngare
ambaye alionekana kuwa na mshtuko mkuu akikataa kuzungumzia jaribio hilo
la kutaka kumuua. “Bado nimeshtuka na siwezi kusema chochote wakati
huu,” alisema katika kituo cha polisi alipoenda kuandikisha taarifa.
Bw Ngare aliahidi kutoa taarifa ya kina baada ya kuhimili mshtuko huo akisema hicho ni kisa cha kushtua.
“Hiki ni kisa
cha kushangaza na nitahitajika kuwa katika hali shwari kabla ya kutoa
taarifa yoyote,” aliongeza huku akifarijiwa na naibu Kamishna wa Kaunti
ya Kirinyaga Bi Roda Onyancha.
Kasisi wa kanisa la Anglikana Samuel Kanjobe ambaye ni mwanachama wa kamati ya CDF alilaani uvamizi huo.
Mkazi wa
sehemu hiyo Bw Maina Kamonde alisema mwanaume huyo alikuwa ameficha
panga ndani ya shati lake kisha akachomoka mbele alipomwona Mbunge
huyo.
Bw Kamonde
aliwakosoa maafisa wa usalama kwa kuzembea kazini. “ Askari wa Utawala
walifahamu kwamba mbunge alikuwa anakagua miradi ya maendeleo shuleni
humo lakini hawakutilia maanani suala hilo, ndio maana wakatoroka kwa
waliposikia milio ya risasi kwa kuwa hakubeba bunduki,” alisema.
Gavana
wa kaunti hiyo Joseph Ndathi alilaani kisa hicho na kuwataka polisi
kufanya uchunguzi wa kina.

Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment