Washiriki
wa warsha ya siku moja ya ujasiriamali mdogo na wa kati katika muktadha
wa fedha iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Taasisi ya
Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF).
SERIKALI imetakiwa kufanya mabadiliko makubwa ya kisera kuwezesha kukua kwa viwanda vidogo na vya kati nchini.Kauli
hiyo imo katika utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na
Jamii (ESRF) kuhusu ukuaji wa sekta hiyo katika muktadha wa upatikanaji
wa fedha.
Akiwasilisha utafiti huo mmoja wa watafiti
Hossana Mpango alisema kwamba kwenye utafiti wao wamebaini mgongano
mkubwa wa kisera na utendaji, unaosababisha kukwama kwa maendeleo ya
sekta hiyo.Alisema ingawa kuna tatizo kubwa la ajira ambalo limefanya
watu wengi kukimbilia kujiajiri wenyewe, kuna changamoto kubwa katika
sekta hiyo hasa sera na uwapo wa mlolongo wa taasisi zinazopishana
mamlaka na huku wakiwa ndio wanatoa leseni.
Alizitaja taasisi hizo zinazopishana
mamlaka kama Shirika la Viwango nchini (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) mamlaka ya kodi (TRA) halmashauri mbalimbali nakadhalika.Alisema
mabadiliko ya kisera yatawezesha kutengeneza muundo unaojali ukuaji wa
sekta hiyo hasa kwa kuangalia kodi zinazolipwa ambazo kwa sasa ni za
aina moja bila kuangalia uwekezaji unaohusika.
Sekta hiyo ya wajasirimali wadogo na wa
kati yenye watu milioni 3 kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2012
inakabiliwa na tatizo la kutokua kutokana na vikwazo mbalimbali vikiwemo
pia kukosekana kwa mafunzo ya ujasirimali na uwezo wa kupata fedha za
mtaji.
“Ni dhahiri upatikanaji wa fedha kutoka nje
ili kuendeleza mtaji ni tatizo. Lakini tatizo hili linakuwagumu zaidi
kutokana na riba kubwa, uchelewefu wa kupata mikopo, rushwa katika
utoaji na ukosefu wa nidhamu ya fedha kwa wakopaji” alisema Hossana.
Alisema pamoja na mambo hayo kuna matatizo
mengine makubwa yanayokwamisha ukuaji wa sekta hiyo. Matatizo hayo
mengine ni gharama kubwa zinaootokana na haja ya kukidhi masharti ya
uendeshaji wa viwanda hivyo vidogo na vya kati, tozo zinazojirudia,
ukosefu wa soko na elimu ndogo ya wajasirimali.
Alisema mabadiliko ya kisera yatasaidia
kuimarisha sheria na kuweka sawa mwelekeo wa sekta hiyo kwa kuzingatia
kwamba inahitaji mchango mkubwa wa nje ili kukua.Alisema mathalani
ingawa kuna SACCOS, taasisi hizo zinashindwa kwenda kukopa kutokana na
riba kubwa na kuwapo kwa mfumo wa kodi na makato mengine yakiwemo ya
tozo usiokuwa na tija.
Alisema suluhu nyingine inayostahili
kufanywa ni kwa taasisi za kifedha kufuata tabia njema za kimataifa za
utoaji wa mikopo unaozingatia pamoja na mambo mengine ukubwa wa mikopo
na malipo kwa kuangalia manufaa ya kiuchumi.
“Ili viwanda
hivi vya chini na kati kukua masuala ya kifedha na yasiyo ya kifedha ni
lazima yaangaliwe na kushughulikiwa…” alisema.Matatizo mengine ni
pamoja na sekta hiyo kukosa msaada huku taasisi mbalimbali zinazohitaji
kushirikiana zikifanya vitu kila mmoja na wake.Taasisi hizo ni SIDO,
TRA, WDF, YDF, BRELA na pia miundombinu inayokera katika maeneo hasa ya
vijijini.
Pia ili kukuza sekta hiyo ni vyema serikali
ikatengeneza miundombinu inayojkidhi haja ya ukuaji wa sekta hiyo kama
maghala, masoko, barabara, maji, umeme kwa lengo la kupunguza gharama za
kufanya biashara.Pia utafiti huo ulishauri kwamba serikali ni lazima
kutenga fungu ambalo litatumiwa na taasisi kama SIDO, NEEC na hata
maofisa biashara wa wilaya kwa ajili ya mafunzo ya ujasirimali na
uendeshaji wa biashara.
Mapema Mkuu
wa idara ya utafiti na machapisho wa ESRF Profesa Fortunata Makene,
aliwataka washiriki wa warsha hiyo kutoa michango katika kuboresha
uelewa ili serikali iweze kutatua kizungumkuti cha ukuaji wa sekta hiyo.
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment