Mwanamke mmoja mkazi wa kata ya Buhare katika manispaa ya Musoma
mkoani Mara Bi Helena Paulo mwenye umri wa miaka 20 amejifungua watoto
wawili mapacha ambao wameungana katika eneo la kifua hadi
tumboni.
Tukio hilo limevuta mamia ya wananchi ambao wamefika katika
hospitali ya rufaa mkoa wa mara mjini musoma kwa lengo la
kutaka kushuhudia tukio hilo.
Akizungumza katika wodi ya wazazi katika hospitali
hiyo ya rufaa ya mkoa wa Mara mjini Musoma, muuguzi wa zamu
Bi Naabu Geraruma, amesema kuwa mwanamke huyo amefanikwa
kujifungua usiku wa saa Saba kwa njia ya Operesheni watoto
hao wawili wenye jinsi ya kike huku wakiwa na uzito wa
kilo 4.6.
Hata hivyo muuguzi huyo wa zamu amesema tukio hilo ni la kwanza
kutokea katika hospitali ya mkoa wa Mara na kwamba hali
za mwanamke huyo na watoto zinaendelea vema na taratibu za
kumpeleka hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza
zimekamika.
Taarifa ambazo zimeifikia Mpekuzi baadaye kutoka jijini Mwanza na
kuthibitishwa na mkurugenzi wa utawala na rasmali watu wa
hospitali ya rufaa ya Bugando Bi Leah Kagine zinasema tayari
mwanamke huyo na watoto wamefikishwa katika hospitali ya rufaa
kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi.

Comments
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment