0


Wakazi wa Butimba, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza  wanahofia kulishwa nyama ya mbwa kufuatia ngozi za mnyama huyo kuokotwa mara kwa mara zikiwa zimechunwa na kuondolewa  kwato. 
 
Hivi karibuni, ngozi nyingine ya mbwa iligundulika saa 5:00 asubuhi eneo la kona ya kuelekea Gereza Kuu la Butimba ambapo wananchi wa eneo hilo walikusanyika kuishuhudia.
 
Hata hivyo, haikuweza kufahamika mara moja nani anahusika na uchunaji wa ngozi za mnyama huyo.
 
 Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye eneo la tukio, baadhi ya wananchi walisema wanahofia kulishwa nyama ya mbwa kwa muda mrefu bila kutambua.
 
Walisema kuonekana kwa ngozi hizo za mbwa mara kwa mara zikiwa zimechunwa ni dalili kuwa biashara ya uuzwaji wa nyama ya mnyama huyo inafanyika kwa kificho.
 
Mmoja watu walioshuhudia ngozi hiyo, Mkushi Hashim alisema majira ya saa 5:00 asubuhi mpita njia mmoja aliiona na kuichukuwa akidhani ya mbuzi, lakini muda mfupi baadaye alibaini ni ya mbwa baada ya kugundua imechunwa kwato. 
 
“Ilikuwa saa tano asubuhi, kuna jamaa alikuwa akipita njiani akaichukuwa ngozi hiyo akidhani ya mbuzi, muda mfupi baadaye akagundua ni ya mbwa,” alisema Hashim na kuongeza:
 
“Kitendo hiki kinaonesha tunalishwa nyama ya mbwa kwa muda mrefu bila kugundua kwani  ngozi hiyo alipoileta kijiweni tulithibitisha kuwa ya mbwa.
 
“Ingekuwa kinachookotwa na mwili sawa, tungesema ngozi inauzwa mahali kwa ajili ya urembo au kuwambia ngoma, sasa kinachookotwa ni ngozi, mwili unakwenda wapi?”
 
Mkazi mwingine wa jiji hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Samwel, alikilaani kitendo hicho na kusema siyo cha kibinadamu.
 
Samwel aliongeza kuwa, watu wanaofanya hivyo ni wauaji na wakitiwa mbaroni wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.
 
“Tunasikia kuna baadhi ya makabila wanakula nyama ya mbwa, lakini siyo kufanya hivyo kwa watu ambao hatuli nyama hiyo, mbaya zaidi ni kwamba mbwa hao wanaweza kuwa na magonjwa ya hatari,” alisema Samwel.
 
Miaka mitatu iliyopita mkoani Pwani, mtu mmoja aliwahi kusulubiwa na wananchi akidaiwa kuwauzia  nyama ya mbwa baada ya kuwalaghai kuwa ni swala.
 
Mwandishi wetu alifika kwenye ofisi za afya za mkoa huo kwa lengo la kuzungumza na wahusika, lakini msemaji hakuwepo ila mfanyakazi mmoja asiyekuwa msemaji alitoa rai kwa wananchi kuwa, wajihadhari na ulaji hovyo wa nyama choma na mishikaki hasa katika sehemu ambazo si rasmi.

Post a Comment

toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment

 
Top

SOMA HABARI KEM KEM KUPITIA BLOG YAKO PENDWA YA HISIA ZA MWANANCHI HAPA

X