Tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza vitendo vilivyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili nchini, imeanza rasmi kazi kwa kupokea taarifa na malalamiko mbalimbali kuhusu operesheni hiyo.
Aidha,
katika kufanikisha majukumu yake, Tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti
wake, Jaji na Balozi mstaafu Hamisi Msumi, itatembelea maeneo mbalimbali
nchini ili kukutana na wananchi wenye taarifa au malalamiko kuhusiana
na jinsi Operesheni Tokomeza ilivyofanyika.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Tume hiyo, Frederick Manyanda katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, jana.
Taarifa
hiyo imeeleza kuwa, taarifa au malalamiko yaliyotokana na utekelezaji
wa operesheni hiyo yatapokelewa kwa njia mbalimbali, zikiwemo kwa posta,
baruapepe na hata simu za mkononi.
Amezitaja
namba zitakazotumika kuwa ni 0714 826 826, 0767 826 826, 0787 826 8265
na 0773 826 826. Aidha, baruapepe ni opereshenitokomeza@agctz.go.tz na
kwa watakaopenda kutoa taarifa au malalamiko kwa njia ya barua,
watalazimika kupitishia barua zao kwa Katibu wa Tume, Tume ya Uchunguzi
wa Operesheni Tokomeza Ujangili, S.L.P 9050, Dar es Salaam.
Tume
hiyo iliundwa na kutangazwa Mei 2 mwaka huu na Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi Ombeni Sefue kuwa, Rais ameunda Tume hiyo kwa mujibu wa kifungu
cha tatu cha Sheria ya Uchunguzi Sura ya 32.
Hatua
ya Rais Kikwete kuunda tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha
Sheria ya Uchunguzi, Sura ya 32 ilikuja baada ya Operesheni Tokomeza
Ujangili kusitishwa na Bunge kutokana ukiukwaji wa sheria na haki za
binadamu wakati wa utekelezaji wake.
Operesheni
hiyo iliyoanza Oktoba mwaka 2013 na kusitishwa Novemba 4 mwaka jana,
ndiyo iliyowang’oa mawaziri wanne kwa kile kilichodaiwa kushindwa
kusimamia vizuri utekelezaji wake.
Mawaziri
hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Wakati
wa kutangaza tume hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
aliyataja majukumu ya tume hiyo kuwa ni pamoja na kuchunguza na kubaini
Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa.
Majukumu
mengine ni kuchunguza na kubaini iwapo Sheria, Kanuni, Taratibu na
Hadidu za Rejea zilifuatwa na watu waliotekeleza Operesheni Tokomeza na
kuchunguza na kubaini iwapo yupo mtu yeyote aliyekiuka Sheria, Taratibu
na Hadidu za Rejea wakati wa Operesheni Tokomeza.
Kuchunguza
na kubaini kama wapo watu wowote waliokiuka Sheria yoyote wakati wa
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na kupima kama hatua zilizochukuliwa
dhidi yao au mali zao zilikuwa stahiki.
Kupendekeza
hatua zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika
kukiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea za Operesheni Tokomeza.
Kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment