0


SUALA la Mahakama ya Kadhi ambalo lilizua mjadala mkali kwenye Kamati za Bunge la Bunge Maalumu la Katiba na kuundiwa kamati ndogo iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hasan, limezikwa rasmi.
 
Hali hiyo imejidhihirisha jana kutokana na kutozungumziwa katika uwasilishaji wa maoni ya walio wengi, wakati kamati hizo zikiwasilisha maoni yake juu ya sura ya tisa na 10.
Imedaiwa kuwa baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo waliweka msimamo wa kutozungumzia kabisa suala hilo.
 
Pamoja na msimamo huo wajumbe walio wachache wa kamati namba nne na tisa, waliliibua wakati wakiwasilisha maoni ya walio wachache.
 
Akisoma maoni ya walio wachache ya kamati namba nne, Ally Omar Juma, alianza kwa kumuomba Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amlinde kwa sababu suala atakaloliwasilisha  halitawafurahisha wajumbe walio wengi.
 
Hata hivyo, mjumbe huyo alipokuwa akisoma taarifa ya walio wachache kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi alionekana kusoma taarifa aliyoiandaa mwenyewe ambayo haikuwamo katika vitabu walivyopewa waandishi wa habari.
 
“Mheshmiwa Mwenyekiti naomba niwasilishe maoni ya walio wachache kama ambavyo tumeyaandaa, lakini naomba univumilie na unilinde pale ambapo litajitokeza jambo ambalo wengine hawatakubaliana nalo.
 
“Maadamu sivunji kanuni na sikiuki Katiba ya Jamhuri ya Muungano, sura ya tisa na ya kumi ndiyo moyo wa Katiba ambayo tunaizungumza katika Bunge hili,” alisema Juma.
 
Alisema Rasimu ya Katiba mpya imeweka msingi imara ambao unawezesha kukuza na kuimarisha Muungano uliopo.
 
“Wajumbe walio wengi wamebadilisha kwa kiasi kikubwa maudhui ya msingi ya rasimu na kuipelekea kuwa dhaifu na kutokuweza kutimiza malengo yake iwapo itapita kama maoni ya walio wengi yanavyosema.
 
“Wajumbe walio wengi wamepunguza na kudhoofisha malengo ya tume hii ya uratibu na uhusiano na kupunguza majukumu ya tume,” alisema Juma.
 
Akizungumzia muundo wa kimahakama, mjumbe huyo alisema mahakama ni chombo kinachotoa haki, hivyo mhimili huo ni muhimu katika taifa.
 
“Hapa nazungumzia uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukiaangalia rasimu ya maoni ya wananchi ukurasa 203 hadi 206, imeelezwa kwa upana namna wananchi walivyotoa maoni yao kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi,” alisema.
 
Alisema kukosekana kwa mahakama hiyo Tanzania Bara kunasababisha adha kwa watu wanaohitaji huduma ya kimahakama na kuwalazimu kwenda Zaanzibar.
 
“Ili kulijenga taifa hili kama Mwalimu Julius Nyerere alivyosema, tunapaswa kutoa haki kwa Waislamu na Wakristo, hili suala la kutugawa tuanzishe Mahakama ya Kadhi ili kuleta haki na kuondoa utaratibu wa watu wa Tanzania Bara kwenda Mahakama ya Mwanzo ambako wanaotoa haki hawafahamu sheria za dini ya Kiislamu,” alisisitiza mjumbe huyo.
 
Alieleza kuwa Katiba ya Zanzibar Ibara ya 19 imeeleza wazi kuwa Serikali haina dini, lakini sheria za Zanzibar zinazungumzia mahakama za Kiislamu na uanzishwaji wa Ofisi ya Mufti inayosimamia misikiti na uendeshaji wa madrasa na urithishwaji wa mali za mwislamu.
 
“Nchini Kenya wenzetu wameanzisha Mahakama ya Kadhi chini ya Katiba ya Kenya ibara ya 178, haijaathiri na Kenya kuna Wakristo wengi kuliko Waislamu, Tanzania tupo sawa kwa sawa na tunaishi kwa amani, hii nchi Baba wa Taifa aliijenga vizuri  iweje leo tugombane kwa kitu kidogo?” alisema Juma.
 
Aliongeza kuwa uanzishwaji wa mahakama hiyo nchini umetajwa na sheria nyingi na katika rasimu ya maoni ya wananchi ukurasa wa 203 imeelezea kwa upana.
 
“Naomba  ninukuu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 haijaanzisha mahakama ya kadhi hata hivyo kutokana na makubaliano ya Serikali na taasisi za Kiislamu mahakama hiyo imeshaanzishwa, sheria mbalimbali za Bunge zinaweka masharti,” alisema.
 
Mjumbe wa kamati namba tisa, Hamis Ally Togwa, akisoma maoni ya walio wachache katika kamati yake, alisema suala la kuanzishwa kwa mahakama hiyo liliibua mvutano mkubwa huku wajumbe walio wengi wakitaka masuala ya taasisi za dini na uendeshaji wake ziwekwe chini ya ibara inayozungumzia uhuru wa imani au dini.
 
“Wajumbe walio wachache katika kamati hiyo wamependekeza kuwa Bunge litatunga sheria kuhusu uanzishwaji na uendeshaji wa Mahakama ya Kadhi ambazo zitakuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri yote ya madai kwa Waislamu wa Tanzania Bara.
 
“Bila kuathiri masharti ibara ndogo ya (3) mambo yanayohusu uendeshaji, gharama pamoja na usimamizi wa mahakama za kadhi utakuwa nje ya mamlaka ya Serikali,” alisema Togwa.
 
MUUNDO WA BUNGE
Awali mjumbe wa kamati namba nne kabla hajazungumzia suala la Mahakama ya Kadhi, alizungumzia muundo wa Bunge na kueleza kuwa katika  Rasimu ya Katiba mpya ilipendekeza idadi ya wabunge wa Bunge la Muungano wawe 75 ili kupunguza gharama za kuliendesha Bunge kama ilivyo hivi sasa.
 
“Wajumbe walio wengi wanapendekeza majimbo ya kawaida ya ubunge na kila jimbo la uchaguzi litoe wanawake na wanaume ambao watafanya Bunge la Muungano liwe na wajumbe 466,” alisema.

Post a Comment

toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment

 
Top

SOMA HABARI KEM KEM KUPITIA BLOG YAKO PENDWA YA HISIA ZA MWANANCHI HAPA

X