Tukio hilo lilitokea Jumamosi iliyopita na kusababisha vifo vya polisi wawili wa kituo hicho na kujeruhi wengine wawili, kufuatia zawadi nono ya Sh. 10,000,000 iliyotangazwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alisema silaha zilizopatikana ni bunduki aina ya Sub Machine Guns (SMG) 11, risasi 158, bastola moja, mabomu 11, magazine 11 na Pump Action tano.
“Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na wasamaria wema hadi kufanikisha kupatikana kwa silaha zote zilizoibwa katika kituo cha Ushirombo Wilaya ya Bukombe wiki iliyopita,” alisema Kamanda Konyo.
Alisema silaha hizo zilipatikana baada ya kufanyika kwa msako mkali ulioanza tangu tukio hilo lilipotokea Jumamosi iliyopita na IGP Mangu aliyekwenda Geita kufuatilia tukio hilo na kuahidi zawadi nono iwapo silaha hizo zitapatikana.
Kamanda huyo alisema tayari Sh. milioni 10 za IGP Mangu ziko tayari iwapo kuna wananchi ambao walitoa taarifa zilizofanikisha kukamatwa kwa silaha hizo na kwamba watanufaika kwa kuwa polisi tayari anwani zao wanazo.
Hata hivyo, Kamanda Konyo hakuwataja watakaogawana bingo hiyo ya IGP, lakini alisema ni wananchi ambao ni siri ya polisi.
MWALIMU AHOJIWA
Aidha, Kamanda Konyo alisema kuwa miongoni mwa watuhumiwa waliohojiwa yumo mwalimu mmoja wa shule ya msingi mkoani Geita, ambaye pia hakumtaja kwa jina.
Alisema hatua za kinidhamu zinaandaliwa kwa maofisa wanaopaswa kuwajibika kiutawala kutokana na tukio hilo bila kufafanua kama walizembea au walihusika.
TUKIO LILIVYOKTOKEA
E 5831 Koplo David Ngupama Mwalugelwana H 627 Mohamed Hassan, walijeruhiwa katika tukio hilo wakati WP 7106 Uria Mwandiga na G 2615 PC Dustan Kimati, waliuawa baada ya kupigwa risasi.
Hata hivyo, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Geita, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, John Temu, aliyeongoza operesheni hiyo na kutambua mazingira ya washukiwa ili kubaini kama kulikuwapo na uzembe wa kiutendaji, alisema watakaobainika watachukuliwa hatua kulingana na taratibu husika.
Jumla ya bunduki 11 za kivita aina ya SMG, bunduki moja aina ya Pump Action 5, ‘Ant riot gun’ moja ya kurushia mabomu ya machozi, bastola moja iliyotengenezwa China, risasi 158, magazine 11 na mabomu 11 ya machozi, yalinaswa katika sehemu tatu tofauti.
Katika kusaka silaha hizo, watuhumiwa wawili walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo huku visu vitatu virefu vikubwa, panga moja na bomu moja la kivita la kurusha kwa mkono vilikamatwa katika maficho ya wahalifu hao.
“Hakuna ubishi huu ni mtandao wa hatari na polisi wanalifahamu hilo na hili tukio la kubwa silaha hizo, kumetikisa usalama na utulivu hasa katika Mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Kagera, Tabora na Geita,” alisema Kamanda Konyo.
Kamanda Konyo alifafanua kuwa Septemba 6, mwaka huu, SMG mbili zilipatikana zikiwa zimefichwa kwenye makaburi kitongoji cha Katete na siku iliyofuata SMG sita na Pump Action moja zilipatikana zikiwa zimefichwa katika tanuru la matofali.
CHANZO:
NIPASHE
Comments
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment