HII NI AIBU, USAFI MPAKA WAGENI WAJE?

Baadhi ya maeneo ya jiji la Dar yakisafishwa kwa ajili ya ujio wa Obama.
Kwanza kabisa tumshukuru Mungu kwa ujio wa wageni lukuki wiki iliyopita na jana, bila shaka waliichagua Tanzania kutokana na amani tuliyonayo.
 Tunamuomba Mungu azidishe amani na mshikamano katika nchi yetu na yule asiyeitakia mema ambadilishe moyo wake urudi katika mstari wa upendo.
Kama nilivyosema hapo juu, wiki iliyopita na jana Jiji la Dar es Salaam limepata ugeni mkubwa sana wa viongozi wa nchi mbalimbali akiwemo Rais Barack Obama.
Ukweli ni kwamba jiji hili ndilo limekuwa mwenyeji wa wageni hao kwa niaba ya nchi na walifanyiwa maandalizi mazito na kusababisha Jiji la Dar kuwa katika hekaheka kubwa za kuandaa mazingira stahiki kwa wageni hao.
Dar es Salaam ni moja ya majiji machafu sana duniani, hivyo kukawa na  juhudi kubwa ya kulisafisha na mamlaka husika ili kuliweka katika hali ya usafi kabla ya wageni hao hawajawasili, hasa Rais Barack Obama wa Marekani ambaye ana ziara rasmi ya kiserikali.
Tumeshuhudia sehemu nyingi za barabara zikitengenezwa usiku na mchana kwa kujengwa upya au kuzibwa mashimo ambayo baadhi yake yalikuwa makubwa sana na kusababisha karaha kwa wananchi waliokuwa wakizitumia.
Katika baadhi ya barabara, mchanga na udongo uliokuwa umezimeza kutokana na kutotunzwa au kufanyiwa usafi kwa muda mrefu, sasa umeondolewa na kuwa safi ajabu!
Takataka zilizokuwa zimezagaa kila kona ya jiji sasa zimezolewa kwa kutumia magari ya halmashauri na ya watu binafsi japokuwa kampeni hiyo ya usafi imesababisha baadhi ya wananchi kupata kero hasa wale waliokuwa wakifanya shughuli zao sehemu ambazo mamlaka haziruhusu maana walivunjiwa vitu vyao.
Ushauri ni kwamba siku nyingine kabla ya kuwavunjia watu, basi waambiwe ili waondoke sehemu hizo badala ya kuwatia hasara maana wengine wamelalamika kuwa mitaji yao imepotea kutokana na vurumai ya kuvunjiwa na mgambo wa jiji.
Ajabu nyingine ni kwamba kuna baadhi ya sehemu madawa ya kuua mbu na wadudu yamenyunyizwa, huku baadhi ya sehemu atakazopita Rais Obama picha zake zimetanda na bendera za nchi mbili hizi.
Harufu mbaya iliyokuwa imeligubika jiji kutokana na uchafu sasa imepungua kwa kiasi kikubwa.
Vijana wa vijiweni nao walijikuta wakipewa ajira ya muda ya kufyeka nyasi, kuzibua na kusafisha barabara na mitaro iliyojaa majitaka. Kwa jinsi walivyofanyakazi kwa bidii utagundua kuwa kumbe wanakaa vijiweni siyo kwa kutaka, bali kwa kukosa ajira.
Pamoja na uzuri huo wa vijana wa vijiweni kupata ajira ya chapuchapu, upande wa pili wa shilingi ni kwamba polisi nao wameendesha kamatakamata ya vijana wengi inaodai ni vibaka, wavuta bangi na vitendo vingine vya kihalifu, huku lengo kubwa lilikuwa ni kusafisha mitaa kabla ya ujio wa Rais Obama.
Ujio wa Obama pia umewafanya Wamachinga kuondolewa katika sehemu alizopangiwa kupita mgeni huyo na ujumbe wake na vibanda vyao vimesambaratishwa na tingatinga za jiji huku meza za biashara zao zikivunjwavunjwa na mgambo wa jiji.
Kama vile hiyo haitoshi, wananchi waishio mikoani nao walitahadharishwa kutokuja Dar es Salaam wakati Rais Obama atakapokuwa jijini kutokana na utabiri kwamba kutakuwa na usumbufu sana, hasa wa foleni barabarani.
Wananchi wengi pamoja na kasoro nyingi zilizojitokeza lakini tumejifunza jambo, kwanza imeonekana kuwa  halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na serikali kuu kumbe wanao uwezo mkubwa wa kulifanya jiji kuwa safi wakati wote.
 Pili, tumeonesha jinsi tunavyojidhalilisha kama taifa kwa kuishi katika mazingira machafu, lakini tunachukua hatua za zimamoto na za harakaharaka za kukimbizana kufanya usafi tunapoona wageni wanatembelea nchi yetu.
Hili jambo liliwahi kukemewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za utawala wake. Alikaripia viongozi wake kwa kufanya usafi wa nyumba alizokuwa akifikia.
“Kila nyumba ninayotembelea inanuka harufu ya rangi, nikawa najiuliza, kwani nyumba hii ni mpya?” namkariri Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere akilalamika wakati wa ziara zake mikoani enzi hizo.
Naamini kwamba kama Mwalimu angekuwa hai haya mambo ya usafi wa zimamoto ni lazima angeyakemea.
Nasema hivyo kwa sababu ni aibu ilioje kwa Watanzania kuishi katika mazingira machafu tukisubiri wageni waje ndiyo tufanye usafi.
Kwa kweli tabia hiyo haifai kwani inaonesha ni jinsi gani tunavyowaona wageni ndiyo wanastahili kuwekwa katika mazingira mazuri na si wenyewe.
Mamlaka husika hazioni umuhimu wa kuwatengenezea wananchi mazingira mazuri kwa kuzoa taka, kutengeneza barabara, kufyeka nyasi, kunyunyizia dawa katika mazalio ya mbu na kadhalika.
Usafi wa mazingira na wa kila mwananchi ni muhimu mno katika ustawi na maendeleo ya binadamu.  Natoa ushauri kwamba ‘gia’ ya usafi iliyofanywa wakati huu wa ziara ya wakubwa hawa iwe hiyohiyo siku zote kwa sababu kuna faida nyingi za jiji kuwa safi na wala hapa sina haja ya kuzitaja kwa sababu viongozi wote wanazijua.
Ieleweke kuwa zoezi la usafi lisiwe Dar tu bali liwe la nchi nzima.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Comments