BAADA ya Televisheni ya Star TV
kutangaza kujitoa kurusha matangazo yao kupitia kingamuzi cha Star
Times, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema sheria na leseni
ya huduma, inazuia kuchukua hatua hiyo.
Hata hivyo, TCRA imesema inafanya
uchunguzi na leo itakutana na uongozi wa Star TV na Star Times,
kuzungumzia suala hilo ili hatua za udhibiti, zichukuliwe kuwezesha
wananchi kupata haki ya msingi ya kupata matangazo ya kitaifa kupitia
televisheni hiyo.
Star TV walitangaza kutoonekana
kupitia Star Times siku chache zilizopita. Uchunguzi wetu umebaini kuwa,
jana waliwasilisha barua ya hatua hiyo kwa kampuni ya Star Times
kupitia mwanasheria wa kampuni yao.
Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent
Mungy aliliambia HabariLeo jana kuwa na wao wamesikia taarifa hiyo
kupitia vyombo vya habari Lakini, alisema Sheria ya Mawasiliano ya
Elektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, haitoi fursa kwa watu wenye
televisheni kujitoa ama kujiweka kwenye ving’amuzi watakavyo.
“Kwa ujumla chaneli zile tano za
kitaifa, zinapaswa kuonekana bure kwenye ving’amuzi vyote, nasi
tumesikia habari hizi na lazima tufanye uchunguzi, lakini pande zote
mbili pamoja na sheria, pia wanafungwa na mkataba wa huduma kwa jamii na
matakwa ya leseni,” alisema Mungi na kuongeza:
“Sheria inawataka wawe na
makubaliano, huwezi kusema mimi najitoa, leseni ina matakwa yake lazima
yafuatwe. Lakini kesho (leo) tutawaita kujua kilichotokea ni nini na
hatua zaidi zitachukuliwa baada ya hapo”.
Aliwahakikishia wananchi ni haki yao
kupata matangazo kupitia televisheni ya Star TV, hata bila kulipia
ving’amuzi, kama ilivyo kwa televisheni nyingine nne za ITV, TBC,
Channel 10 na EATV.
Msaidizi wa Meneja wa Star Times,
Hellen Elisa alithibitisha kujitoa kwa Star TV. Alieleza ni kweli
walipokea barua mbili juzi, zikieleza kuhusu hatua yao hiyo kwamba
wamejitoa kwa matakwa yao.
“Walituletea barua jana (juzi)
kupitia mwanasheria wao wa kampuni, wao ni wamiliki wa chaneli, na sisi
tunahusika kurusha matangazo, jambo lolote kama hili likitokea lazima
kwanza kutii sheria, tumewasiliana na TCRA na wakubwa wetu wa kazi
wametueleza kuwa wanalishughulikia kwa karibu,” alisema Elisa.
Kwa upande wake, Msimamizi wa masuala
ya Ving’amuzi wa Sahara Media Group, wamiliki wa Star TV, Steve Diallo
alipoulizwa kwa simu kuhusu kujitoa kwao Star Times, alisema yeye si
Msemaji na kumtaka mwandishi kuwasiliana na watu wengine.
Miezi kadhaa iliyopita, Clouds TV
nayo ilijitoa, lakini ikarejea tena. Jana, Mkurugenzi wa Utafiti wa
Redio Clouds FM, Ruge Mutahaba alisema sheria inawabana wamiliki wa
televisheni za kijamii kujitoa na wanapaswa kuonekana katika ving’amuzi
vyote.
HabariLeo

Comments
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment