UONGOZI wa Simba umechukua uamuzi wa
kumpandisha kizimbani kiungo mshambuliaji, Mrisho Ngassa kutokana na
uamuzi wake wa kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga.
Habari za uhakika kutoka ndani ya
Simba zimeeleza kuwa, Msimbazi wameamua kufanya mambo yao kimya na
wameamua kutumia mahakama ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine.
“Hakika sasa tumeona suala hili si la
kufanya kama filamu, maana wenzetu (Yanga) pamoja na Ngassa wameamua
kutufanyia uhuni. Wachezaji wanataka kufanya Simba ni kama sehemu ya
kuchota fedha na kuondoka.
“Kitu kibaya zaidi tumegundua system
(mfumo) ya soka imekuwa ikiwalinda sana kutokana na ushabiki mkubwa
uliopo katika kamati zilizo chini ya TFF. Sasa sisi tumeona bora
kuchukua hatua zaidi,” kilieleza chanzo cha uhakika.
“Tutamfikisha Ngassa mahakamani,
tutadai zaidi ya Sh milioni 200 kama sehemu ya kutaka fidia kutokana na
mkataba tulioingia naye. Mkataba upo, msione tumekaa kimya mnaona kama
hatuna cha kusema.
“Ila sasa tumeamua kufanya mambo kwa
mfumo tofauti na leo (jana) usiku tutakuwa na mkutano kwa ajili ya
kujadili kuhusiana na suala hili na tutajua lini rasmi apande
kizimbani.”
Championi Jumatano ndiyo lilikuwa la
kwanza kuandika kuhusiana na Ngassa kusaini Yanga miaka miwili na
kueleza kila anachopata katika mkataba wake, achana na wale waliosema
katika stori yao eti anatarajia kusaini.
Kwa mujibu wa chanzo hicho kutoka
ndani ya Simba, mkataba kati ya Ngassa ulipelekwa na kusajiliwa TFF
tangu Desemba, mwaka jana.
Tayari baba yake (soma Uk 2)
amezungumzia kuhusiana na mwanaye kuhamahama na Yanga imeshatangaza
kumtambulisha kwa mashabiki Juni 3 (soma Uk 2).
Suala la Ngassa kutua Yanga limezua
gumzo kubwa na huenda likazua mgogoro mkubwa baina ya timu hizo mbili.
Mwishoni mwa mwaka jana, Ngassa
alitua Simba kwa mkopo akitokea Azam, lakini akakabidhiwa gari aina ya
Toyota Verossa na Sh milioni 30 na Simba kutangaza imemuongezea mkataba
wa mwaka mmoja baada ya kumalizika kwa mkopo, lakini Ngassa mwenyewe
amekuwa akisisitiza hana mkataba na Msimbazi baada ya ule wa Azam
kumalizika.
Comments
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment