
Rais Jakaya Kikwete amemwagia sifa
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hatua ambayo inaweza kutafsiri
mengi katika medani ya siasa nchini.
Akizungumza na wabunge wa CCM kwenye
Ukumbi wa White House Dodoma juzi, Rais Kikwete ambaye pia mwenyekiti wa
chama hicho,alisema nguvu za Lowassa pekee zinatosha kushinda uchaguzi
mdogo wa kiti cha udiwani Kata ya Makuyuni kilichoko wilayani Monduli.
Kata ya Makuyuni iko wilayani
Monduli, ambako Lowassa amekuwa mbunge wake tangu mwaka 1995.
Habari za kutoka ndani ya kikao hicho
zinaeleza kuwa Rais Kikwete alitoa kauli hiyo kuhusu kampeni za
uchaguzi huo wa Makuyuni, baada ya kuwa ametoa ruksa kwa makada wa chama
hicho wanaotaka urais kuanza kujipitisha pitisha miongoni mwa wanachama
wa chama hicho.
Lowassa anatajwa kuwa miongoni mwa
wanaCCM wanaotaka kumrithi Rais Kikwete kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
“Sina tatizo na pale Makuyuni, najua
muscles (misuli) za Mzee Lowassa zinatosha kutupa ushindi; au vipi
mzee?”alidokeza mmoja wa wabunge wa CCM akimnukuu Rais Kikwete.
Uchaguzi wa Udiwani Kata ya Makuyuni
unaotarajiwa kufanyika Juni 16, mwaka huu, utakuwa wa ushindani mkali
kati ya CCM na Chadema ambao historia yao kisiasa mkoani Arusha ni ya
uhasama.
Katika uchaguzi huo, unaofanyika
baada ya kifo cha Abdillah Warsama (CCM), chama hicho kitatetea nafasi
yake kwa kumsimamisha Godluck Lerunya na Chadema ni Japhet Sironga.
Mbali na Kata ya Makuyuni, uchaguzi
wa udiwani mkoani Arusha utafanyika pia katika Kata za Kaloleni, Themi,
Kimandolu na Elerai, kutokana na waliokuwa madiwani wa kata hizo
(Chadema), kufukuzwa na chama chao.
“Mnaweza kuchafuana leo, kesho
mkapata mgombea mwenye nundu nyingi na mabandeji kila mahala, halafu
mkapata shida kumnadi,” alisema.
Siyo mara ya kwanza kwa Kikwete
kumsifia Lowassa kwani aliwahi kufanya hivyo mwaka jana huko Longido
wakati akikabidhi ng’ombe.
Pia aliwahi kumsifia wakati wa
kampeni za uchaguzi za mwaka 2010 wakati Kikwete alipomwelezea Lowassa
kama Mbunge makini na kuwaomba watu wa Monduli kumchagua tena.
Hata hivyo, alipoulizwa kama baada ya
kuruhusiwa kuanza kujipitisha kwa wanaCCM kama anataka kuwania urais,
Lowassa alijibu kupitia watu wake wa karibuni kuwa asingependa
kuzungumzia suala hilo hasa baada ya Rais kutoa kauli hiyo.
Kutangaza nia ruksa
Rais Kikwete aliwaeleza wabunge hao
kuwa si kosa kwa watu kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi ikiwamo urais mwaka 2015.
“Wabunge na mawaziri wenye nia ya
kutangaza nia ya kugombea urais wawe huru, kwani hiyo ni haki yao,
isipokuwa wafanye kwa wema bila kukivuruga chama na kuwagawa wanaCCM
katika makundi. Sioni tatizo watu kujipitisha. Sisi sote hapa
tulijipitisha. Lakini tufanye hivyo kistaarabu bila kuvurugana.”'
Aliwaagiza wabunge wa chama hicho
kwenda majimboni mwao kusikiliza kero za wananchi badala ya kusubiri
wakati wa uchaguzi.
Kauli ya Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye naye anatajwa kuwa miongoni mwa
wagombeaamewataka waandishi waache kuandika kila siku habari za urais na
badala yake waandike mambo ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana baada ya kukutana na mabalozi wa nchi zinazoendelea kuhusu Mkutano
wa Smart Partnership, unaotarajiwa kufanyika nchini, Membe alisema ni
vizuri yakaandikwa mambo ya maendeleo na si kila wakati kuandika mambo
ya urais.
“Mkutano kama huu nchi kama Kenya
watauripoti vizuri na kwa undani hivyo mfanye hivyo si kila kitu urais
2015,”alisema Membe.
Mkutano huo utaanza Mei 28, hadi Juni
Mosi na utajadili jinsi gani sayansi na teknolojia vinaweza kutumika
kuzikwamua kiuchumi.
Comments
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment