Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda jana Jumamosi, Machi 2, 2013 amezindua Tume maalum
aliyoiunda ili ifanye uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne
yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu na kuwataka wajumbe wa Tume hiyo
watafute kiini cha mserereko wa kushuka kwa ufaulu kuanzia mwaka 2010
hadi 2012.
Waziri Mkuu
amezungumza na wajumbe wa Tume hiyo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri
Mkuu, Magogoni, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.
Amesema
kwa mujibu wa hadidu za rejea, wajumbe wa tume hiyo watatakiwa
kuangalia ni sababu zipi zimechangia kuwepo kwa matokeo hayo mabaya,
mserereko wa kushuka umekuwa ukiongezeka kwa sababu gani, usimamizi
katika Halmashauri ukoje, ukaguzi wa elimu na uhamishiwaji wa sekta ya
elimu kwenye Wizara ya TAMISEMi umechangiaje kushuka kwa kiwango cha
ufaulu.
Vilevile,
watatakiwa kuangalia mitaala na mihutasari ikoje, kuangalia uwiano
uliopo kwenye mitihani inayotungwa ikiwa ni pamoja na uhakiki wa
mitihani hiyo; kuangalia mazingira ya kufundishia, mfumo wa upimaji,
usimamizi na uendeshaji, na kutokuwepo kwa chakula shuleni kunachangiaje
kushuka kwa utendaji mbaya wa wanafunzi katika masomo yao.
Tume hiyo yenye
wajumbe 15, imepewa muda wa wiki sita kuanzia Machi mosi iwe
imekamilisha kazi hiyo na kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri Mkuu.
Tume itaongozwa
na Prof. Sifuni Mchome wa Tume ya Vyuo Vikuu, na Makamu wake
atakuwa Bi. Bernadetha Mushashu (Mbunge wa Viti Maalum – Kagera).
Wajumbe ni Bw. James
Mbatia (Mbunge wa kuteuliwa), Bw. Abdul J. Marombwa (Mbunge
wa Kibiti), Prof. Mwajabu Possi (Chuo Kikuu – UDSM), Bibi Honoratha
Chitanda (CWT), Bibi Daina Matemu (TAHOSSA) na Bw. Mahmoud
Mringo (TAMONGSCO).
Wangine ni Bw. Rakhesh
Rajani (TWAWEZA), Bw. Peter Maduki (CSSC), Mwl. Nurdin
Mohamed (BAKWATA), Bw. Suleiman Hemed Khamis (Baraza la
Wawakilishi, Zanzibar), Bw. Abdalla Hemed Mohamed (Chuo Kikuu –
SUZA), Bw. Mabrouk Jabu Makame (Baraza la Elimu Zanzibar na Bw. Kizito
Lawa (Taasisi ya Kukuza Mitaala).
Comments
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment