Viongozi CCM watakiwa kutatua kero zao

Viongozi CCM watakiwa kutatua kero zao

Geita.

Chama cha Mapinduzi kimesema migogoro iliyopo ndani ya chama hicho inasababishwa na baadhi ya viongozi kufanya kazi bila kufuata misingi ya chama kwa kufukuzana, kunyoosheana vidole na kueneza majungu badala ya kujadili changamoto zinazowakabili wananchi.

Utatuzi wa changamoto za wananchi, utasaidia wananchi kuendelea kukiamini chama hicho ambacho kilikuwa kikikabiliwa na mgawanyiko kutokana na baadhi ya viongozi wasio waaminifu kukigawa kwa kujali masilahi yao binafsi.

Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Nape Nnauye akifungua kikao cha kwanza cha halmashauri kuu ya chama hicho mkoani Geita amesema umefika muda muafaka kwa viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa kubadilika kwa kufanya kazi wakitumia misingi na kanuni zinazotokana na maamuzi ya vikao.

Katibu wa CCM mkoa wa Geita Shaib Akwilombe amesema katika mkutano huo wa kwanza wa halmashauri kuu ya CCM watajadili mambo muhimu ikiwemo semina kwa wajumbe ambapo baadhi ya viongozi wa serikali wameshirikishwa.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Joseph Msukuma amezungumzia suala la uchaguzi wa wajumbe wa kamati ya siasa wa mkoa huo ambao umepangwa kufanyika jumapili wiki hii na kusema kwamba kamati yake haina kundi lolote miongoni mwa wagombea.

Mkutano huo wa siku mbili ni wa kwanza mkoani Geita tangu kuanzishwa kwa mkoa huo mwaka jana.

Comments