HII NI RIPOTI JUU YA TAJIRI ALIYE UAWA RUNZEWE
POLISI wa Mkoa wa Geita wametumia nguvu kuzuia msafara wa
waombolezaji waliokuwa na mwili wa marehemu mfanyabiashara, Yemuga
Fungungu (48), mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha vurugu kubwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo alikuwapo wakati askari
wake walipoingilia msafara huo na kusababisha vurumai kubwa.
Waombolezaji hao walikuwa wakiuhamisha mwili wa marehemu Fungungu kutoka
Hospitali ya Runzewa kuupeleka katika Hospitali ya Geita.
Sakata hilo la ndugu na polisi lililotokea saa nane mchana juzi Jumamosi
katika Pori la Samina, Geita na polisi wakiwa kwenye magari matatu
wakiwa wamesheheni silaha mbalimbali walifika na kuzuia mwili wa
marehemu kusafirishwa.
Baadhi ya ndugu wa marehemu akiwamo mkewe, wanadai kwamba Fungungu
alifariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi wanaosemekana kwamba
walimvamia nyumbani kwake usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita kisha
kupora mamilioni ya fedha. Wanadai kwamba alipigwa risasi tumboni na
kichwani katika Kijiji cha Runzewe, Wilaya ya Bukombe mkoani hapa.
Katika tukio hilo inadaiwa kuwa kiasi cha Sh360 milioni kiliporwa. Kati
ya fedha hizo, Sh60 milioni zinadaiwa kwamba zilikuwa kwenye gari wakati
Sh300 milioni zilikuwa kwenye masanduku mawili yaliyokuwa ndani ya
nyumba.
Pia ndugu hao walidai kwamba Sh1.2 milioni zilichukuliwa na askari
wawili wa kiume baada ya kumpekua mke wa marehemu kwenye nguo za ndani.
Pia askari hao wanadaiwa kupora mali mbalimbali za marehemu zikiwamo
redio mbili, video kamera moja, nguo za marehemu ikiwamo kanzu, mashine
ya printer, mashine ya inventor, karatasi za picha, deki mbili za
kucheza CD, pamoja na nguo za mke wa marehemu.
Mapema Kamanda Paulo alikuwa ameeleza kuwa marehemu alijiua mwenyewe
baada ya kumjeruhi Polisi, Fortunatus Beatus kwa risasi lakini taarifa
hizo zimepingwa vikali na ndugu na jamaa wa marehemu ambao wanadai
marehemu aliuawa na polisi akiwa nyumbani kwake.
Polisi kuzuia waombolezaji
Baada ya polisi kuyasimamisha magari manane yaliyokuwa katika msafara
huo wa kupeleka mwili wa marehemu kwenda kuhifadhiwa katika chumba cha
maiti Hospitali ya Geita, kulizuka mabishano makali kati ya Kamanda
Paulo na ndugu wa marehemu.
Inadaiwa kwamba polisi walikuwa wakishinikiza mwili huo urejeshwe
Runzewe, Bukombe kwa kuwa tayari ulikuwa umefanyiwa uchunguzi jambo
ambalo liliwakera waombolezaji hao.
Kabla ya kamanda huyo kufika eneo hilo, msafara huo ulisimamishwa na
Polisi wa Usalama Barabarani ambao walikuwa wamefuatana na wale wa
Kutuliza Ghasia (FFU), wakiongozwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha
Wilaya ya Geita, Leonard Makona.
Baada ya kuusimamisha msafara huo, Makona aliwataka ndugu wa marehemu
kumsubiri Kamanda Paulo ambaye alifika baada ya takriban dakika 10.
Mwandishi wa habari hii ambaye alikuwa katika eneo la tukio, alishuhudia
ndugu wa marehemu na Kamanda Paulo wakirushiana maneno.
“Mnapeleka wapi mwili wa marehemu, ina maana hamkuridhika na uchunguzi
wa daktari wa Bukombe?” alihoji kwa ukali na kujibiwa pia kwa ukali na
kaka wa marehemu, Mariatabu Fungungu: “Kwa nini mnatusimamisha? Tunaomba
tuite waandishi wa habari hapa ili waje washuhudie tukio hili. Kwa nini
msikae ofisini?”
Baadaye, kamanda huyo aliwaamuru askari wake kuwaingiza katika gari la
polisi ndugu watano wa marehemu wakiwamo mke wa marehemu, Lucia Kilaza
(23) na Mariatabu. Walifanya hivyo kwa kutumia nguvu na kisha kuondoka
nao hadi katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita.
Ndugu wa marehemu walilalamikia kitendo hicho wakisema kilikuwa na lengo
la kuficha ukweli wa tukio hilo.
Mke wa marehemu
Kilaza alidai kuwa kifo cha mumewe kilitokea baada ya zaidi askari 20
kuvamia nyumbani kwake yapata saa tisa usiku na kumwamuru Fungungu
kutoka nje na alipogoma, ndipo walipoanza kupiga risasi na kuvunja vioo
vya madirisha na milango na risasi kumpata marehemu. Pia alidai kuwa
walipiga mabomu ya machozi.
Alisema baada ya tukio hilo, walivunja mlango na kuingia ndani kisha
kumchukua mumewe ambaye tayari alikuwa amefariki na kumtupa nje... “Mimi
pia walinichukua wakanitupa nje ya uzio baadaye wakaanza kunipekua nguo
za ndani na kuchukua Sh1.2 milioni ambazo nilikuwa nimezificha baada ya
kuona wameanza kufyatua risasi.”
Wakizungumzia tukio hilo, Mbunge wa Bukombe, Profesa Kalikoyela Kahigi
na Diwani wa Runzewe, Yusufu Fungameza walisema Serikali inatakiwa
kuingilia kati suala hilo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za
kisheria waliohusika katika tukio.
Alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, Kamanda Paulo aliwaahidi waandishi
wa habari kwamba angelitolea ufafanuzi jana Jumatatu. Hata hivyo,
alishindwa kufanya hivyo kwa madai kwamba anapisha kwanza uchunguzi wa
mwili wa marehemu kwenye Hospitali ya Geita.
Ndugu wa marehemu wamegoma kuuzika mwili wa marehemu wakitaka uchunguzi
wa kina ufanyike kwa kutumia jopo maalumu la madaktari huku wakiitaka
Serikali kuunda tume kuchunguza tukio hilo.
Comments
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment