FAMILIA ya Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo
Milionea’ aliyefariki dunia Novemba 26, mwaka huu kwa ajali ya gari
iliyotokea Songa-Kibaoni, Muheza, Tanga imemteua msanii wa vichekesho
Musa Kitale kuwa mwangalizi wa mali za marehemu, Amani limejuzwa.
Akizungumza na paparazi wetu
jijini Dar hivi karibuni, Kitale alisema familia hiyo imemteua yeye kwa
kigezo cha ukaribu wake na marehemu tangu zamani.
Alisema amepewa jukumu la kuhakikisha
mikataba yote ambayo marehemu aliifanya na makampuni mbalimbali
inakwenda vizuri sanjari na kuangalia mali kama vile gari na samani za
ndani ya nyumba.
“Nimeambiwa nisimamie mikataba, niangalie
mali za mshikaji (Sharo) kwa kipindi chote cha kusubiria arobaini ya
marehemu ambayo itafanyika Januari 4, 2013 kijijini alikozikwa,”
alisema Kitale.
Kitale alisema baadhi ya mikataba
anaifahamu kwa vile yeye ndiye aliyekuwa shahidi, “lakini wa DTV
aliosaini siku tano kabla ya kufariki dunia (hakuutaja) inabidi
aushughulikie Muddy Suma jamaa aliyemuazima gari marehemu,” alisema.
Kuhusu kwenda kuzima taa katika nyumba
aliyokuwa akiishi marehemu, Sinza Palestina Dar, Kitale alisema:
“Kwa kipindi hiki ambacho tunasubiri
arobaini ya marehemu ifike ni ngumu mtu kwenda kufungua mlango ili
azime taa, namuomba mama mwenye nyumba avumilie kwani zoezi la kufungua
mlango wa kwa Sharo ni hadi familia yake iwepo hapa Dar na si mimi
peke yangu.”
Akakumbuka jambo hili: “Tulishtushwa na
taarifa tulizozisoma kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi iliyopita kuwa,
kuna rafiki mmoja wa marehemu alikwenda pale nyumbani na kutaka
kutapeli vitu vya marehemu, kama isingekuwa msimamo wa mwenye nyumba
jamaa angefanikisha utapeli wake ndiyo maana haraka sana familia
ikanipa mimi jukumu hili.”
Comments
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment