Nilimaliza wiki iliyopita nikiwa
naelezea kipengele cha kutafakari kabla ya kuamua.
Hupaswi kufanya uamuzi ambao baadaye
utakuja kubaini kuwa kuna eneo ulikosea. Makosa yako yatakufanya ujute.
Kwa nini ujute? Kila siku unapopatwa na
jambo, unapaswa kutafakari
kabla ya kuamua. Ukijijengea kanuni hiyo, utafika mbali katika maisha
yako ya uhusiano. Siyo kimapenzi tu, bali pia hata kijamii.
Uamuzi
wa jazba, kukimbilia kuacha ni tatizo lingine. Hapo sasa kirusi
kinaweza kuwa wewe mwenyewe. Unatakiwa kujiangalia kwa makini mno. Pima
kiwango chako cha hasira na tukio lenyewe halafu jikosoe. Jitahidi
kupiga moyo konde mara nyingi iwezekanavyo.
Penda sana kujirudi, uamuzi wa kuacha
uje baada ya kujiridhisha
kwamba hakika mwenzi wako uliyenaye hawezi kukidhi viwango vya moyo
wako. Uwe umejitahidi kumkosoa na kumsahihisha mara kadhaa. Ukiwa na
tabia ya kuacha na kukimbilia kuanzisha uhusiano mpya, maana yake wewe
ni kirusi.
Ni kweli kuwa mlango wa furaha
unapofungwa, mwingine hufunguliwa
lakini mara nyingi huwa hatujui thamani ya kitu tunachopata au
tulichonacho mpaka pale tunapokipoteza. Sasa usifike huko, fanya
upembuzi na uchambuzi wa kina. Heri kumsahihisha leo kwa udhaifu wake
mdogo ili baadaye akupe furaha kamili na ya kudumu, kuliko kumuacha
kisha ujute kwa miaka mingi wakati akiwa ameshakupa kisogo.
Naendelea kukubali kuwa kumpa mtu
mapenzi yako yote haimaanishi naye
atakupa au atakurejeshea kwa kiwango kilekile ambacho wewe umekitoa.
Zingatia kwamba umeamua kupenda, usipende kwa matarajio ya kwamba naye
atakupenda na kukujali kwa kiwango unachokiwaza.
Timiza wajibu wako, ukiona hakupi
unachotaka tambua kwamba unayo
nafasi ya kumuelewesha kile ambacho anatakiwa kukifanya ili ufurahie
mapenzi yake. Fanya kazi nzuri kila siku, tambua kwamba wanaofanikiwa
katika maisha ya kimapenzi ambao leo wanajisema wanakula bata ni wale
walioamini katika kufundisha.
Pengine kuna vitu unavyotegemea
kuvisikia au kuvipata kutoka kwake
lakini haujaambulia chochote. Kabla ya kukimbilia kumtoa kasoro kwamba
hakufai, hebu jiulize mwenyewe, ni lini ulimwambia unachopenda kusikia
kutoka kwake? Umetaka awe anakwambia anakupenda, je, wewe umemwambia
unampenda mara ngapi?
Usidai kile ambacho wewe mwenyewe
hutekelezi. Unataka mwenzi wako awe
anaonesha hisia za juu pindi mnapokuwa faragha, je, wewe huwa
unamuonesha hizo hisia? Utagundua kwamba wewe unadai kile ambacho
hukitekelezi kwake. Pengine hakuoneshi kwa kuamini hupendi.
Upo kwenye uhusiano, inapita miezi
mitano hujawahi kumtamkia mwenzi
wako neno “nakupenda”. Siku moja unajitahidi, unajitutumua unamwambia
mpenzi wako “nakupenda sana my sweet love”. Kutokana na ugeni wake,
anakujibu “asante.” Sasa jibu lake linakukera nini?
Ingekuwaje kama ungemwambia hivyo halafu
naye akakujibu “najua”, si
ndiyo pangechimbika. Mapenzi yanahitaji moyo wa subira. Akikujibu
“asante” au “najua”, chukulia kwamba yote ni majibu, unachotakiwa
kufanya ni kumfanya mwenzi wako atambue jibu la kukupa ili uwe na
furaha. Wengine haya mambo ni ‘mashokolo mageni’, kwa hiyo hawajazoea.
Unaweza ukafanya uamuzi halafu baadae
ukajutia, usiseme kwa heri kama
unajisikia kuendelea, usiseme humpendi mtu tena kama unajua huwezi
kumuacha aondoke . Hii ndiyo sababu ya kukutaka uishinde jazba.
Amekuudhi leo, hebu lala kwanza ili kesho ulitafakari tukio ndiyo utoe
uamuzi.
Kumbuka inachukua dakika kumuona mtu na
kumtamani, ila baada ya huyo
uliyemtamani, ukimuingiza ndani ya moyo wako na kumpenda, ni ngumu
kumsahau. Wapo wanaoteseka maisha yao yote kwa kushindwa kuwaondoa
kwenye vichwa vyao wale ambao waliachana nao. Wengine, hugharimu kabisa
maisha yao. Acha jazba, uamuzi wako wa hasira leo, unaweza kukutuma
kubwia sumu. Mimi nimeyaona
Comments
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment