0

sta
NIPASHE
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele, amesema iwapo rasimu ya Katiba inayopendekezwa haitasambazwa na kuwafikia wananchi kote nchini mapema, atatangaza kuwahamasisha  wasiipigie kura ya maoni.
Kura ya maoni ya wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa rasimu ya katiba hiyo inatarajiwa kupigwa Aprili, mwaka huu, lakini hadi kufikia jana, ilikuwa haijaanza kusambazwa kwa wananchi.
Askofu Mengele alisema hayo katika hafla ya kukabidhi Shule ya Sekondari ya Ruhuji iliyokuwa chini ya Balozi mstaafu wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Gidion Ngilangwa.
Alisema amezunguka sehemu nyingi nchini, lakini hajaona mahali ambako wananchi wanakosema kuwa wanaifahamu katiba hiyo.
“Sisi kama kanisa hatutakubali kuwaruhusu wananchi kupigia kura katiba inayopendekezwa kama haitafikishwa kwa wananchi, kwani wanatakiwa kuisoma na kuielewa kabla ya kuipigia kura:-Askofu Mengele.
Alisema kanisa linajiuliza itakapofika Aprili 30, mwaka huu wananchi watapigia kura ya ndiyo au hapana juu ya nini wakati hawajui kilichopo ndani ya katiba hiyo.
NIPASHE
Wakazi wa Feri, Dar es Salaam, wameiomba Serikali kukifanyia marekebisho kivuko cha MV Magogoni kinachofanya safari zake kati ya Kivukoni na Kigamboni  ambacho kimekuwa kinaharibika kila mara na kusababisha usumbufu kwa abiria.
Hatua hiyo imefuatia matukio ya kuharibika mara kwa mara nyakati za usiku na kuchukua  muda majini huku kikiwa na abiria na magari.
Fadhili Mbaga, mkazi wa Kigamboni,  alisema, Serikali  inapaswa kuangalia kwa makini suala la usalama wa abiria wa Feri ambao wanatumia usafiri huo, kutokana na kivuko hicho kutokuwa na sifa za kusafirisha abiria wengi na mizigo kwa wakati.
Abiria tumekuwa na wasiwasi na huu usafiri kwani mara nyingi injini ya kivuko hiki siyo nzima na kusababisha ofu kubwa kwetu:-Mbaga.
NIPASHE
Jeshi la Polisi limekumbwa na dhahama nyingine baada ya  askari wake wawili wa mkoani Tabora, kupewa kipigo kwa madai ya kusababisha kifo cha kijana mmoja wa mjini humo.
Tukio hilo lilitokea juzi sambamba na tukio la kuuawa kwa askari wawili wa kituo polisi cha Ikwiriri, wilayani Rufiji, Pwani.
Aidha, Jeshi la Polisi limeungana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuwasaka watu waliovamia Kituo cha Polisi Ikwiriri wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani na kuwaua askari hao na kupora silaha mbalimbali zikiwamo bunduki na risasi.
Katika tukio la Tabora, kijana huyo anadaiwa kufa wakati akifukuzwa na askari hao wa Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Tabora kwa lengo la kutaka kumtia mbaroni kwa tuhuma za  kushiriki mchezo wa kamari.
Kamanda Suzan Kaganda aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni  PC Yohana na MW Daniel Isonda na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kitete  kutokana na kujeruhiwa kwa kipigo na wananchi.
MTANZANIA
KIKAO cha pamoja kilichowakutanisha viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kimetoa mikakati ya pamoja ikiwamo kuandaa ratiba ya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya urais kwa kila chama.
Hatua hiyo imekuja baada ya kikao cha siri cha siku mbili kilichowakutanisha viongozi wa juu wa Ukawa ambao ni Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Dk. Emmanuel Makaidi (NLD).
Viongozi hao wamekubaliana kuweka mikakati hiyo ikiwamo ya kushika dola katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Katika kikao hicho, viongozi hao wametoa ratiba ambayo inakitaka kila chama kuteua mgombea wake wa urais ili ajulikane mapema kabla vikao vya Ukawa kuteua jina la mgombea mmoja.
Imewekwa mikakati hii kwa lengo la kuimarisha demokrasia kwa kila chama husika, hasa vinavyounda Ukawa vipate muda wa kutosha wa kuweza kufanya uteuzi mapema.
Lakini pia sasa ni wakati kwa wale wazalendo wa kweli, hasa kutoka upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wana uchungu na nchi yao wajitoe mapema na kuja kushiriki uchaguzi kupitia Ukawa badala ya kusubiri hadi mwisho, kwani wakifanya hivyo wanaweza wakakuta milango imefungwa.
MTANZANIA
ENEO la viwanja vya Anatouglou jijini Dar es Salaam, jana lilikumbwa na vurugu wakati wa kuapishwa kwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa mitatu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilala.
Katika vurugu hizo aliyekuwa mgombea wa CCM, Mtaa wa Kigogo Fresh B, Kata ya Pugu, Mariano Haruna, alijikuta akipata fedheha baada ya kudhalilishwa kwa kuvurumishiwa matusi, kukunjwa na kuchaniwa shati lake.
Haruna, alifanyiwa vitendo hivyo na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliofika kwa lengo la kushuhudia uapishaji huo.
Vurugu hizo, zilizosababisha mvutano mkubwa kati ya wasimamizi wa uchaguzi wa Manispaa ya Ilala na wananchi, zilianza taratibu wakati washindi wa nafasi ya uenyekiti na wanakamati wa mitaa yao walipokuwa nje ya ukumbi huo wakisubiri kuapishwa.
Kadiri majina ya wenyeviti hao yalivyokuwa yakiitwa kwa ajili ya kuingia ndani kuapishwa, ndivyo presha ya wafuasi wa vyama mbalimbali waliofika kushuhudia shughuli hiyo ilivyozidi kupanda.
Hali ilibadilika baada ya jina la aliyekuwa mgombea wa Mtaa wa Kigogo Fresh B, Haruna kuitwa, badala ya yule wa Chadema, Patricia Mwamakula ambaye wananchi walimtaka.
Wakati Haruana akielekea kuingia ndani, wananchi walimzuia na kumvuta nje, hatua iliyowafanya wasimamizi wa uchaguzi kwa kushirikiana na polisi nao kumvuta huyo kuingia ndani ya ukumbi.
Hata hivyo, baada ya mabishano na mvutano huo uliodumu kwa dakika kadhaa, wananchi waliwashinda askari hao na wasimamizi wa uchaguzi na kufanikiwa kumtoa nje.
Baada ya kutolewa nje, askari na wasimamizi walimgeuka na kumwamuru aondoke kwa ridhaa yake hadi Mkurugenzi atakapomwita tena.
HABARILEO
KATIKA kutekeleza moja ya malengo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hususan kuwatafutia ajira Watanzania nje ya nchi, Wizara hiyo kupitia Ubalozi Mdogo wa Tanzania uliopo Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu umefanikisha kulishawishi Shirika la Ndege la Emirates kuajiri Watanzania wengi zaidi kuanzia mwaka 2015.
Emirates, moja ya mashirika ya ndege tajiri zaidi duniani, linamiliki zaidi ya ndege za kisasa 280, huku likiwa na safari za uhakika duniani kote.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Simba Yahya alisema shirika hilo litaajiri Watanzania katika kada mbalimbali.
Wamekubali kuajiri Watanzania katika kada mbalimbali, ambapo maofisa wake wanaosimamia ajira watakuja nchini (Tanzania) Machi 2015 kwa ajili ya kuwafanyia usaili Watanzania watakaoomba kazi hizo na kupata uteuzi wa awali:-Yahya.
Aliwataka Watanzania kuchangamkia ajira hizo, ambazo awali zilitangazwa Julai 2014, lakini ni Watanzania wachache tu walioomba na hivyo kutofikia lengo lililokusudiwa.
JAMBOLEO
BOMBA la gesi lililopo mkoani Mtwara lipo hatarini kusombwa na maji kutokana na mmomonyoko wa ardhi uliotokea eneo la kiwanda cha kuchakata gesi mkoani hapa.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limetumwa magari 30 mkoani humo ili kurahisisha kazi ya kudhibiti mmomonyoko huo ambao unatishia uhai wa bomba hilo.
Mkuu wa Brigedia katika mikoa yote ya kusini, John Chacha alitoa kauli hiyo jana wakati akizumngumza na waandishi wa habari hatua iliyofikiwa katika kudhibiti mmomonyoko huo.
Alisema tatizo linalowakabili ni la vitendea kazi ikiwemo makoleo, sepetu na zilizopo ni 15, magari makubwa ya kusomba mawe kutoka eneo la Msijute ikiwa ni kilomita 80 kutoka eneo la tukio.
Mkuu huyo alisema tatizo hilo wamelifikisha makao makuu ya jeshi pamoja na Wizara ya Ulinzi na Usalama ambapo magari 30 ya jeshi yapo njiani kwenda eneo. Alisema kulikuwa pia na tatizo la mafuta, lakini tayari wamepatiwa lita 10,000.
Zimebakia mita 4 tu maji kufika katika eneo la bomba na kuweza kuling’oa na kazi iliyofanyika ni mzuri na hadi hivi sasa tayari mita 150 kutoka eneo lililokuwa msitu zimeondoka:-Chacha.
MWANANCHI
Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuanza mjini Dodoma, sasa hakuna shaka kwamba Rais Jakaya Kikwete atafanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri wakati wowote kuanzia leo na kabla ya Jumapili (saa 48) kutokana na kukabiliwa na safari ya nje.
Rais anatarajiwa kufanya mabadiliko hayo baada ya kumwondoa Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow baada ya kuingiziwa Sh1.6 bilioni kwenye akaunti yake.
Mwingine ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye anatuhumiwa kutoshughulikia kwa makini sakata hilo na kusababisha Serikali kupoteza fedha hivyo kuwapo kwa uwezekano mkubwa wa kumvua uwaziri utakaomlazimu Rais kufanya mabadiliko madogo kwenye baraza lake, ikiwa ni miezi isiyozidi mitano kabla ya kuvunja Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Rais anaondoka Jumapili kwenda Davos (Uswisi kuhudhuria mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi la Dunia (WEF)), hivyo kwa jinsi yoyote ile ni lazima atangaze baraza kesho (leo) au Jumamosi,” alisema mpashaji habari wetu.

Post a Comment

toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment

 
Top

SOMA HABARI KEM KEM KUPITIA BLOG YAKO PENDWA YA HISIA ZA MWANANCHI HAPA

X