Baada ya taji la Miss Tanzania kuvishwa kwa mshindi wa pili, utata mwingine umeibuka baada ya mrithi huyo, Lilian Kamazima kudaiwa kuwa si raia.
Jana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii
kulikuwa na taarifa zinazodai kuwa Lilian siyo raia wa Tanzania na
kwamba anatokea Rwanda.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Lino
International Agency ambao ndiyo waandaaji wa mashindano ya Miss
Tanzania, Hashim ‘Uncle’ Lundenga alisema tuhuma hizo kuhusu Lilian siyo
kweli.
“Sisi tunajua Lilian ni Mtanzania, tunaangalia
cheti cha kuzaliwa alichotuletea kamati yetu ambacho kinaonyesha
alizaliwa Tanzania, pia ni Mtanzania, hayo yanayosemwa kwamba Lilian
siyo Mtanzania hatuyajui kabisa,” alisema Lundenga.
Pia Lundenga alisema kitendo cha Sitti Mtemvu
kujivua taji la Miss Tanzania 2014 kumemnyima sifa ya kuendelea
kushikilia taji la Miss Temeke na lile la Kitongoji cha Chang’ombe.
“Sitti amevua taji la Miss Tanzania maana yake ni
kwamba hata lile la Miss Temeke 2014 na lile la Miss Chang’ombe 2014
ambayo ndiyo alikuwa mshindi kabla ya kushinda lile la taifa, ameyavua
pia,” alisema Lundenga.
Sitti aliingia katika kashfa ya tuhuma za
kudanganya umri baada ya nyaraka zake mbalimbali kuonyesha amezaliwa
1989 na siyo 1991 kama alivyowasilisha kwenye kamati ya Miss Tanzania.
Kwa mujibu wa sheria za mashindano hayo, mshiriki anatakiwa awe na umri wa kuanzia miaka 18 na usiozidi miaka 24.
Mwandaaji wa mashindano wa Miss Temeke, Ben Kisaka
alisema, “Waliotoa taarifa ya Sitti kujivua taji ni kamati ya Miss
Tanzania, hivyo wao ndiyo wanapaswa kutoa taarifa zingine kuhusu taji la
Temeke.”
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment