Rais Jakaya Kikwete amesema anaomba yasimkute ya Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliyeshambuliwa katika mdahalo wa katiba uliofanyika Dar es Salaam, juzi.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo Mwanza jana katika
mkutano wa 12 wa Shirikisho la Taasisi za Kupambana na Rushwa (Safac)
unaojumuisha nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(Sadc).
“Naamini Katiba Inayopendekezwa itapitishwa,
nina matumaini hayo. Nadhani na mimi nitakavyokuwa napiga kampeni
hayatatokea yale ya jana(juzi), maana mie sioni haya kuipigia kampeni
kama wale wenzetu ambao wanataka isipite,” alisema Rais Kikwete kwa
ufupi.
Juzi, Jaji Warioba alishambuliwa na kundi dogo
la watu walioingia katika mdahalo ulioitishwa na Taasisi ya Mwalimu
Nyerere na kutolewa chini ya ulinzi.
Vurugu hizo
zilitokea wakati Jaji Warioba alipokuwa akihitimisha hotuba yake kwa
kuhoji watu wanaotumia vibaya jina la Mwalimu Julius Nyerere kupitisha
hoja zao katika misingi isiyokubalika.
Miongoni mwa
wanaotuhumiwa kumshambulia Jaji Warioba ni Katibu wa Hamasa wa Jumuiya
ya Umoja wa Vijana (UVCCM), Paul Makonda ambaye hata hivyo, jana alikana
kufanya kitendo hicho.
Tukio lakemewa kila kona
Wasomi,
wanasiasa na wananchi wa kada mbalimbali nchini wamelaani vurugu
zilizotokea katika mdahalo huo na zaidi, kitendo cha Jaji Warioba
kuvamiwa na kupigwa.
Mbali na kulaani, mjumbe wa
iliyokuwa Tume hiyo, Profesa Mwesiga Baregu alimtaka Rais Kikwete kutoa
tamko, huku wanaharakati na wasomi wakitaka ulinzi uimarishwe kwa
viongozi wa kitaifa wakiwamo wastaafu.
Profesa Baregu alisema ni vizuri kwa Rais akatoa tamko kuhusu tukio hilo ili kunusuru mchakato mzima wa Katiba Mpya.
“Nashangaa
mpaka sasa Serikali imekaa kimya licha ya kutokea kwa tukio hili la
aibu kwa Taifa, ambalo unaweza ukahisi lilipangwa ili kuhatarisha
usalama wa wananchi,” alisema na kuongeza:
“Jaji
Warioba kwa wadhifa wake, anatakiwa kupatiwa ulinzi wa kutosha kama
walivyo viongozi wengine wastaafu, lakini cha kushangaza jana (juzi)
mpaka tunaanza mdahalo hakukuwa na askari hata mmoja ndani ya ukumbi,
badala yake walikuwa nje ya jengo lile.”
Alisema kwa
mwenendo uliopo sasa, itakuwa vigumu kupatikana Katiba Mpya kwani
wananchi wanakoseshwa haki zao za msingi ikiwamo usalama.
Mwenyekiti
wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee alilaani
kitendo hicho na kuitaka Serikali kuwachukulia hatua kali waliohusika.
Akihutubia
mkutano wa hadhara katika Kata ya Nyalikungu Wilaya ya Maswa mkoani
Simiyu, Mdee alimtuhumu Makonda na wenzake kuwa wamefanya tukio ambalo
limeidhalilisha nchi.
“Tunalaani vikali kilichomtokea
Warioba ...nani asiyefahamu uadilifu wa Warioba? Eti wanampiga, hili
hatuwezi kukubali litokee tena. Serikali iwachukulie hatua kali kwani
waliofanya wanajulikana kwa nini kuwaficha au kosa la Warioba ni lipi?”
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema
viongozi wa kitaifa wanatakiwa kupewa ulinzi wa kutosha na kitendo
kilichotokea juzi ni aibu kwa Taifa zima.
Mwenyekiti wa
PPT - Maendeleo, Peter Mziray alisema viongozi wastaafu wasijihusishe
kabisa na masuala ya kisiasa badala yake wapumzike kama alivyoamua
Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikataa kuzungumzia lolote akisema yupo nje ya nchi.
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Katiba la Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema vurugu
hizo ni maafa na uhuni wa kutisha unaostahili kulaaniwa.
“Sitaki
kuamini kuwa wale vijana wahuni walitumwa na CCM, sitaki kuamini hata
kidogo… hali ile ni maafa. Ulinzi na usalama umekwisha kabisa,” alisema
na kuongeza: “Hii hali ya kusubiri mpaka maafa yatokee haifai. Warioba
ana mlinzi mmoja na sisi jana tulikuwapo pale ilifikia kipindi hadi
walinzi wa Jukata waliingia kumsaidia Warioba, ni aibu kubwa.”
Mtafiti
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Patience Mlowe alisema
vurugu hizo zimemshangaza kila mpenda amani na demokrasia.
“Ni
fedheha kwa Taifa. Warioba ni Makamu wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu,
halafu vijana wanashindwa kumheshimu… hili ni janga kwa Taifa,” alisema
Mlowe.
Mbunge wa zamani wa Vunjo, Aloyce Kimaro alisema
kitendo alichofanyiwa Jaji Warioba hakijawahi kufanywa tangu nchi ipate
uhuru na kwamba waliofanya kitendo hicho wanataka kuharibu utawala wa
Rais Kikwete ambaye amewapa Watanzania uhuru wa kuzungumza.
“Hao
wahuni waliompiga Warioba walionekana vizuri kwenye runinga. Serikali
iwachukulie hatua kali kwa kuwa wamedhalilisha nchi, pia Watanzania
tujifunze kusikiliza maoni ya mtu hata kama yanakukera,” alisema.
Mwasisi
wa Chadema, Edwin Mtei aliwataka Watanzania kulaani kitendo hicho huku
akimtaka Jaji Warioba asikate tamaa, bali aendelee kutetea maoni ya
wananchi.
Mtei alisema kilichofanyika ni sawa na laana
kwa vijana kwani haiwezekani kuwashambulia wazee wenye heshima kubwa
katika Taifa bila sababu za msingi.
CUF kulinda midahalo
Chama
cha Wananchi (CUF) mbali ya kulaani, kimekwenda mbali na kikisema
kinachukua dhamana ya kuilinda midahalo yote itakayomhusu Jaji Warioba,
waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko Katiba na Taasisi ya Mwalimu
Nyerere (MNF), kwa nia njema ya kutoa elimu ya uraia juu ya Katiba
Inayopendekezwa.
Taarifa ya Naibu Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Abdul Kambaya ilisema chama hicho
kimeamua kuchukua dhamana hiyo kwa kuwa polisi wameshindwa kutekeleza
wajibu wao.
“Jaji Warioba ni kiongozi wa Taifa hili,
hivyo kwa namna yoyote ile hawezi kudhalilishwa huku CUF kama wadau wa
mambo ya siasa na elimu ya uraia tukiwa kimya,” ilisema taarifa hiyo ya
Kambaya.
Makonda ajitetea
Wakati
wanasiasa na mitandao ya kijamii ikimlaani Makonda, kiongozi huyo jana
aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusema hakumpiga Jaji
Warioba, bali alikuwa akimwokoa katika vurugu hizo.
Makonda
alisema baada ya vurugu hizo kutokea, aliamua kumwokoa Mjumbe wa
lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba, Amon Mpanju na Jaji Warioba ili
wasijeruhiwe kwenye vurugu hizo. Picha zilizochapishwa jana
zilimwonyesha Makonda akiwa amemshika Jaji Warioba.
“Nilipoingia
ukumbini nilikwenda kukaa jirani na Mpanju, baada ya kutokea vurugu
nikaona ni lazima nimwokoe kwa sababu ya ulemavu wake wa kutokuona. Jaji
Warioba alituona na akanisogelea akaniambia nisimwache Mpanju asije
akapata matatizo. Kwa hiyo nikawa niko karibu na Mpanju na Warioba ili
kuhakikisha kuwa wanakuwa salama.”
“Warioba ni kama
baba yangu, kamwe siwezi kunyanyua mkono wangu na kumpiga, nitakuwa
ninajitafutia matatizo, huu ni mchezo mchafu unaochezwa na baadhi ya
wanasiasa wenye lengo la kunichafua.
“Leo (jana)
asubuhi Warioba amenipigia simu akinipa pole kwa vurugu hizo, nami
nikampa pole kwa yote yaliyotokea jana, sasa inakuwaje mtu uliyempiga
halafu akakupigia simu ya kukupa pole?” alisema Makonda.
Hata
hivyo, Jaji Warioba hakupatikana jana kuzungumzia nini hasa kilitokea
kati yake na kada huyo wa CCM ambaye pia alikuwa mjumbe wa Bunge la
Katiba.
Kauli ya Polisi
Msemaji
wa Polisi, Advera Bulimba alisema bado viongozi wastaafu wanapatiwa
ulinzi wa kutosha lakini hakutaka kufafanua zaidi vigezo vinavyoangaliwa
kwa kile alichoeleza kuwa ni sababu za kiusalama,” alisema.
Mwaka 2009 Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi alipigwa kibao shavuni alipokuwa akihutubia katika Baraza la Maulid.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema watu kadhaa
ambao hata hivyo hakuwataja kwa majina wala idadi, walihojiwa ili kujua
chanzo cha vurugu hizo na kuwa uchunguzi unaendelea.
Chanzo: MWANANCHI
Chanzo: MWANANCHI
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment