SIERRA Leone jana ilianza siku tatu
za kujifungia ndani kwa wananchi wote, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na
kusambaa kwa ugonjwa wa ebola.
Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya nchi
hiyo, raia wake wapatao milioni sita wameamriwa kutotoka ndani usiku na
mchana hadi kesho, ikiwa ni hatua ya kuruhusu uchunguzaji wa ugonjwa
huo kuwa rahisi.
Madaktari wasio na mipaka pamoja na
wataalamu wengine wa tiba wanapita nyumba hadi nyumba kuchunguza iwapo
kuwa mgonjwa wa ebola ili kumpeleka kwenye kituo na kuondoa uwezekano wa
kuambikiza wengine.
Ugonjwa wa ebola umeziathiri nchi za
Afrika Magharibi, ikiwemo Sierra Leone, Nigeria, Liberia, Guinea ambapo
zaidi ya watu 2,630 hadi sasa wamekufa kwa ugonjwa huo usio na tiba wala
kinga huku wengine 5,357 wakiambukizwa ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani
(WHO), ugonjwa huo ni miongoni mwa magonjwa hatari duniani ya mlipuko,
tangu virusi vya ugonjwa huo vilipigundulika mwaka 1976 na kwamba kwa
miezi sita iliyopita ugonjwa huo umeua zaidi kuliko miaka 38, iliyopita.
Madaktari wasio na mipaka walisema sio
rahisi kwa wataalamu wa afya nchini humo kugundua wagonjwa wote wa ebola
ila ni lazima wataalamu wa masuala ya ebola washirikishwe zaidi ili
kuja na suluhu la ugonjwa huo.
“Kunahitajika vitanda vya kutosha kwenye
vituo vya wagonjwa wa ebola ili kusaidia kudhibiti tatizo hili,”
walisema madaktari hao.
Wakati huo huo, miili nane ya wananchi
imekutwa kwenye eneo moja kijijini nchini Guinea, ambapo kati ya miili
hiyo ipo ya waandishi wa habari watatu.
Miili hiyo ilikutwa na timu ya watu waliokwenda vijijini kuelimisha wananchi kuhusu ugonjwa huo.

Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment