Uvumi wa kuwapo kwa watu wanaoteka nyara watoto kwa kutumia magari aina ya Noah, umeleta mtafaruku katika shule saba za msingi Manispaa ya Temeke, na kusababisha wazazi kuvamia shule hizo na kufungwa kwa muda.
Hata hivyo, katika baadhi ya shule hizo kumeripotiwa kutokea vurugu
kiasi cha jeshi la polisi kuingilia kati kutawanya watu waliotaka
kuvunja mageti ya kuingilia kwenye shule hizo.
Taarifa za kuwapo kwa matukio ya watoto kutekwa na watu wasiojulikana
zilianza kuenea wiki tatu zilizopita, ambapo shule zilizoathirika ni
Chekeni Mwasonga, Mikwambe, Rangi Tatu, Mchikichini, Charambe,
Kiburugwa, Jitihada na Mbagala Kuu.
Akizungumza na NIPASHE Jumamosi, Afisa Elimu ya Msingi Manispaa ya
Temeke, Honorina Mumba, alisema uvumi huo siyo wa kweli na hawafahamu
nani anahusika kuusambaza na kwa madhumuni gani.
Alikiri kwamba kazi ya utoaji huduma katika baadhi ya shule umekuwa
mgumu baada ya wanafunzi kutofika shuleni kufuatia wazazi wao kuwazuia
wakihofia usalama wa watoto wao.
MATUKIO YALIVYOJIRI
Mumba alisema taarifa ya kuwapo kwa watu wanaoteka nyara zilianzia
katika Shule ya Msingi Mwasonga, ambapo ghafla zilisambaa kwa kasi
kutoka shule moja hadi nyingine kiasi ambacho sasa inakuwa ngumu
kudhibiti.
Imearifiwa katika matukio hayo kila shule kuna watoto kati ya wanne hadi
sita walitekwa nyara katika mazingira ya kutatanisha na watu
wasiojulikana ambao wanatumia magari ya Noah kwa ajili ya kutimiza
vitendo hivyo.
“Hata mimi nashangaa uvumi huu unavyoenea kwa kasi na kusababisha kazi
ya utoaji elimu kuwa ngumu, tunajitahidi sana kuwaelimisha wazazi lakini
kila siku shule moja hadi nyingine inaathirika,” alisema.
Alisema Uongozi wa Manispaa ya Temeke kwa sasa unashirikiana na walimu
na Jeshi la polisi, kuhakikisha wanajitahidi kutuliza taharuki katika
shule hizo.
WALIMU WAKIRI HALI NI MBAYA
Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili, baadhi ya walimu na viongozi
wa serikali za mitaa, walisema hali imekuwa mbaya katika shule hizo
baada ya wanafunzi kutohudhuria masomo kufuatia wazazi wao kuwazuia.
Mwenyekiti wa mtaa Rangitatu, Said Pazi, alisema toka siku ya Jumatatu
ilipotokea tukio hilo, hali imekuwa ya wasiwasi kwa wanafunzi hao,
ambapo baadhi yao wameshindwa kuhudhuria masomo kikamilifu.
Alisema siku ya tukio, kulikuwa na wakati mgumu baada ya wazazi
waliokuwa na taharuki kuvamia shule hiyo na kutaka kuvunja geti kuu la
kuingilia ndani, kushinikiza wapewe watoto wao baada ya kusikia kuna
wanafunzi watatu wametekwa nyara.
“Nikiwa hapa ofisini wananchi walikuja na kuniambia kuna watoto
wametekwa, lakini kila nikijaribu kuuliza mazingira ya tukio hilo,
hakuna aliyeweza kueleza kwa usahihi, hata hivyo idadi ya watu ilipozidi
kuongezeka na kuhatarisha amani ilibidi tuwaite polisi watusaidie,”
alisema Pazi.
Kwa upande wa shule ya msingi, Jitihada ilibidi ichukuliwe hatua ya
kufungwa shule kwa siku moja baada ya wazazi kuamua kuwachukua watoto
wao kwa nguvu na wengine kukimbia ovyo baada ya kuenea taarifa ya
kutekwa wanafunzi sita.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Odenary Mosha, alisema tukio hilo limetokea
juzi majira ya saa 4.30 asubuhi, wakati wanafunzi wakiwa mapumziko.
Alisema walijaribu kuwatuliza wazazi hao, lakini ilishindikana baada ya
kuanza kuvamia madarasa kwa nia ya kuwatafuta watoto wao.
Hata hivyo, Mosha alisema hakuna mwanafunzi aliyeripotiwa kupotea na
hata mzazi aliyefika kusema mtoto hajarudi nyumbani kwao. Mwalimu mkuu
wa Shule ya Msingi Kiburugwa, Mponda Shabani, alisema kwa ujumla
wanafunzi wake wote 3,400 wapo salama na hakuna taarifa yoyote ya
kupotea miongoni mwao.
Hata hivyo, Afisa Elimu mama Mumba, aliwashauri wazazi kuacha kusikiliza
maneno ya mitaani na kueleza katika shule zote kunafanyika zoezi maalum
la utoaji wa elimu wa kujitambua kwa wanafunzi.
DC: SINA TAARIFA
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, alipotafutwa kwa kutumia simu
yake ya kiganjani, alisema bado hajapata taarifa kuhusu matukio hayo na
kwamba analifanyia kazi.
KAMANDA KIENYA: NI WANAFUNZI WATORO
Kamanda Mkoa wa kipolisi wa Temeke, Kienya Kienya, akizungumzia suala
hilo, alisema jambo hilo limezushwa na baadhi ya wanafunzi wasiopenda
shule kwa lengo la kusababisha hofu kwa wenzao.
Alisema jumla ya shule nne eneo la Mbagala zimeathirika kwa siku mbili pekee.
Hata hivyo, kamanda huyo alisema kwamba yupo mbioni kushirikisha vyombo
vya habari kuhakikisha uvumi huo unamalizika ili kuondoa usumbufu kwa
wanafunzi.
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment