RAIS Jakaya Kikwete amesisitiza msimamo wa Serikali, kwamba mashine za elektroniki za ukusanyaji kodi (EFDs), lazima ziendelee kutumika nchini. Alisema hayo jana wakati alipozungumza kwenye uzinduzi wa Ofisi za Mamlaka ya Bandari (TRA) mjini Karatu katika Mkoa wa Arusha, na kuongeza kuwa changamoto za mashine hizo zinajadilika.
“Najua
kuna maneno mengi kuhusu suala hili. Kwa hiyo maelekezo yangu ni kwamba
kaeni chini, mjadili matatizo yaliyopo na kupata ufumbuzi. Kama ni
suala la bei pia linazungumzika lakini tunahitaji mfumo huu wa malipo ya
kodi,” alisema.
Aliagiza
viongozi wa TRA kukaa chini na wadau na watumiaji wa mashine hizo
kuzungumza na kutafuta majawabu yanayolalamikiwa na wadau.
Alisema
kuacha kutumia mashine hizo ni kurudi nyuma kwa kuwa zimeshaanza
kutumika duniani kote na hata nchi jirani baadhi zimeshaanza kutumia na
nyingine ziko katika maandalizi ya kutumia.
“Kwenye
hili tusirudi nyuma kwa sababu tukifanya hivyo, tutakuwa tunarudi nyuma
sana kwa sababu dunia nzima inaelekea huko na hata majirani zetu wote
ama wameanzisha mfumo huo ama wanajiandaa kuuanzisha.”
“Hatuwezi
kurejea kwenye mfumo ule wa kutumia vijirisiti. Mfumo wa sasa unaifanya
kazi ya kukusanya kodi kuwa rahisi kwa Serikali yenyewe na kwa walipa
kodi. Najua watu hawapendi kulipa kodi lakini hakuna njia ya jinsi ya
kuendelea isipokuwa kwa kulipa kodi,” alisisitiza Rais Kikwete.
Kwa
muda mrefu TRA imekuwa ikisisitiza kuwa utaratibu wa kutumia mashine za
EFDs ulianzishwa kwa lengo la kumrahisishia mfanyabiashara utunzaji wa
kumbukumbu za biashara za kila siku pamoja na kuondoa usumbufu wakati wa
ukadiriaji wa kodi. Mfumo huo wa kutumia mashine za kodi za
kielektroniki ulianza kutekelezwa kwa awamu.
Awamu ya kwanza ilianza mwaka 2010 kwa wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Awamu
ya pili ilianza 2013 ikiwahusu wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa
kwenye VAT ambao mauzo ghafi kwa mwaka ni Sh milioni 14 na zaidi.
Kwa
mujibu wa taarifa za TRA, wafanyabiashara zisizo rasmi zikiwemo za mama
lishe na wale wanaotembeza bidhaa barabarani, hawahusiki kwa sababu
hawana sehemu maalumu ya kufanyia biashara.
Miongoni
mwa wafanyabiashara wanaotakiwa kutumia mashine hizo ni wenye maduka ya
vipuri, mawakili, maduka ya jumla, wafanyabiashara wakubwa wa mbao,
migahawa mikubwa, maduka ya simu na vipuri vyake, baa na vinywaji
baridi, studio za picha, biashara za kutoa huduma za chakula, wauzaji wa
pikipiki, maduka makubwa ya nguo na biashara zinginezo Kwa mujibu wa
taarifa za TRA, kwa nchi nzima walengwa ni wafanyabiashara laki mbili tu
kwa awamu ya pili kati ya wafanyabiashara zaidi ya milioni moja na nusu
ambao wamesajiliwa kulipa kodi.
Rais
Kikwete alikuwa katika ziara ya siku moja kukagua shughuli za maendeleo
wilayani Karatu katika Mkoa wa Arusha na leo atafanya ziara kama hiyo
ya siku moja katika Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro
Credit: Habari leo
Credit: Habari leo
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment