Hatimaye modo maarufu Bongo, Jacqueline Fitzpatrick
‘Jack Patrick’ amepandishwa kortini kwa mara ya kwanza huko Macau nchini
China, Aprili 10, mwaka huu kwa kukutwa na madawa ya kulevya tumboni
aina ya heroin kete 57 au kilo 1.1 yakiwa na thamani ya zaidi ya
shilingi milioni 223 huku ishu kubwa kwa muda wote aliokuwa mahakamani
ikiwa ni kuangua kilio kila wakati.
Jack alipandishwa kwenye korti hiyo ikiwa ni mara yake ya kwanza
tangu alipokamatwa na madawa ya kulevya ‘unga’ Desemba mwaka jana
akitokea Bongo kupitia Thailand na kuingia nchini humo.
ILIKUWAJE?
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini
kilichopo Macau, Jack alifikia hatua hiyo dakika 15 baada ya kupanda
kizimbani na kukutana na nyuso za Wachina tu zikimwangilia.
“Yeye alijua angekuta Wabongo au hata watu weusi wakimpa kampani,
lakini matokeo yake alikutana na sura za Wachina tu,” kilisema chanzo
chetu.
Kikaendelea: “Unajua kwa kawaida mtu anapopanda kizimbani mara zote
anafarijika sana endapo atawaona anaowafahamu, hasa ndugu zake ambao
watafika kumtia moyo, sasa yeye hakulipata hilo.”
DAKIKA 10 ZATUMIKA KUMSOMEA MASHITAKA
Kuna madai
kwamba, msoma mashitaka wa mahakama hiyo alitumia dakika 10 kutokana na
taratibu za kisheria za huko huku akitakiwa kusema ndiyo au hapana tu
kabla keshi hiyo kupigwa kalenda hadi Mei 23, mwaka huu.
KUNA MADAI ALIZOMEWA
Chanzo hicho kiliendelea
kudai kwamba, mbali na kukutana na upweke huo mahakamani, pia Jack
alipata kisanga kingine pale baadhi ya raia wa nchi hiyo walipomzomea
kwa sauti ya chini wakati akitoka kortini.
Inadaiwa kuwa, kwa Wachina kumzomea au kumsema vibaya mtu aliyedakwa
na madawa ya kulevya ni kawaida kwani hakuna biashara, inapigwa vita
nchini humo kama ya unga wakiamini unaangamiza nguvu kazi ya kizazi
kijacho.
NDUGU WADAIWA KUMKATIA MAWASILIANO
Habari
nyingine kutoka chanzo chetu zilidai kwamba, kwa sasa Jack amebaki yeye
na Mungu wake baada ya nduguze waishio Bongo kumkatia mawasiliano kwa
kile walichodai kuwa kitendo alichokifanya kimeiaibisha familia nzima.
“Unajua ndugu zake walikata mawasiliano kabisa? Nchi nzima au tuseme
dunia nzima kilio ni jinsi vijana wanavyoharibika kwa madawa ya kulevya,
sasa kule kubainika kwamba Jack alibeba unga tumboni kwenda kuuza
kumeifanya familia kujisikia vibaya sana,” kiliongeza chanzo hicho
kikiomba chondechonde kisitajwe .
KAMA ATARUDI BONGO SALAMA
Habari zaidi zinadai
kwamba modo huyo ambaye pia ni Miss Ilala No 3, 2005, aliwahi kumwambia
mshirika wake mmoja akiwa mahabusu kwamba, kama atabahatika kurejea
Bongo salama, atakwenda kupiga dua juu ya kaburi la mama yake ili amsimamie katika
kumwondolea nuksi kama siyo mabalaa. Baba wa Jack anadaiwa kuishi nje ya
nchi.
TUJIKUMBUSHE
Jack alikamatwa Desemba 19, mwaka
jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Macau nchini China akitokea jijini
Bangkok nchini Thailand kuelekea Guangzhou, Mji Mkuu wa Jimbo la
Guangdong Kusini mwa China ambako ilidaiwa ndiko alikokuwa anafikisha
unga huo.
Ilidaiwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyochangia kukamatwa kwake ni
kuonesha uso wenye uchovu, kuanza kuwa na hali mbaya ya mwili, kushindwa
kujibu maswali vizuri na hati yake ya kusafiria, yaani ‘passport’
kukutwa imegongwa mihuri ya kuingia nchini humo kila mara jambo ambalo
wakaguzi waliliona si la kawaida kwa msichana kama yeye.
Source: Gazeti la Risasi Mchanganyiko/gpl
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment