NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe amesema kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania analipwa sh milioni 384 kwa mwaka, sawa
na sh milioni 32 kwa mwezi pasipo kukatwa kodi.
Hii ni mara ya pili kwa Zitto kutangaza hadharani
mishahara ya viongozi wakuu wa serikali, akiwa ameanza na ule wa Waziri
Mkuu, aliyesema analipwa takribani sh milioni 26 kwa mwezi.
Akiwahutubia wananchi mjini Igunga
jana, ukiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha chama Kanda ya
Magharibi, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini alisema kuwa
sababu ya kutaka mishahara ya viongozi wakuu wa nchi ijulikane, ni
kuzuia mianya ya watu wachache kuiibia nchi kutokana na usiri wa jambo
hilo.
Zitto alisema hoja ya msingi si kiasi wanacholipwa
viongozi hao walioajiriwa na wananchi, bali ni usiri unaofanywa juu ya
kiwango hicho jambo alilosema kuwa linaweza kutumiwa na wajanja
kuendelea kuinyonya nchi.
Alisema ni jambo la kusikitisha
kuona mwalimu anayelipwa mshahara wa sh 220,000 kwa mwezi akikatwa kodi,
huku viongozi wa kuchaguliwa wakiwa wanapokea mishahara mikubwa pasipo
kukatwa kodi licha ya kuhudumiwa kila kitu na serikali.
Aliongeza kuwa katiba ya sasa
Ibara ya 43(1), inaeleza kuwa rais atalipwa mshahara pamoja na malipo
mengine, huku ibara hiyo hiyo kifungu cha pili ikizuia mshahara na
marupurupu kupunguzwa, hali aliyoelezea kuwa ni muhimu katiba mpya
ikabadilisha sheria hizo kwa manufaa ya nchi.
“Kwa hiyo hata kesho kama Dk.
Willibrod Slaa akiwa rais na akataka kupunguza mshahara wake, kwa katiba
hii hawezi na hili jambo si sahihi kwani viongozi wa ngazi hizi
wanapata kila kitu bure kutoka serikalini,” alisema Zitto.
Akiwa katika Kata ya Choma, Zitto
alikagua kilichokuwa kiwanda cha kuchambulia pamba cha Giner ambacho
kimeacha kufanya kazi tangu mwaka 1998.
Alisema kufa kwa viwanda vingi vya
uzalishaji nchini kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ya Rais
mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, akidai kuwa alishindwa
kutofautisha suala la uwekezaji na biashara huru.
“Ni serikali ya Mkapa ndiyo
ilitufikisha hapa katika kupotea kwa viwanda nchini, wao walidhani
biashara huru ni kuwapa wawekezaji viwanda vyetu na serikali kujiweka
pembeni, sasa nchi imebaki kutegemea uchumi wa uchuuzi badala ya
uzalishaji,” alisema.
Alisema sera ya uwekezaji katika Serikali ya CCM
ilichukuliwa kama fursa ya viongozi wa chama hicho kujinufaisha na mali
za serikali pasipo kujua wataendeleza vipi.
Zitto alisisitiza kuwa kila mara
CHADEMA imekuwa ikisisitiza bungeni juu ya kupiga marufuku usafirishaji
wa pamba kwenda nje kama malighafi, na badala yake wakitaka viwanda
vifufuliwe kwa ajili ya kutoa ajira kwa Watanzania.
Alirejea kusisitiza sera ya
hifadhi ya jamii kwa wakulima akisema imefikia wakati serikali kupitia
SSRA ione umuhimu na ulazima wa kuhakikisha wanaongeza Watanzania wenye
hifadhi ya jamii kwa kuanza mfumo maalumu wa hifadhi ya jamii kwa
wakulima (Supplementary scheme for social security to small holder
farmers).
“Ninapendekeza serikali ichangie nusu kwa nusu na mkulima
ili kuvutia uwekaji akiba katika nchi na kuwa na sera ya uwekezaji
katika maeneo yatakayomwinua mkulima kama miundombinu ya umwagiliaji,
mikopo nafuu kwa wakulima kwenye pembejeo na nyumba na bima ya afya.
“Nimezungumzia umuhimu wa uwazi
katika matumizi ya fedha za umma ikiwemo malipo ya watumishi na viongozi
wa umma. Nimewaeleza wananchi wa Nzega kuwa siku ya Jumanne kamati
yangu ya Hesebu za Serikali (PAC) itaanza kukagua mahesabu ya vyama vya
siasa nchini,” alisema.
Zitto alisema vyama vya siasa vinatumia fedha za umma
takribani sh bilioni 20 kila mwaka kama ruzuku, kwamba ni haki ya
wananchi kujua fedha zinatumika namna gani.
Alisema kuwa wananchi wa Nzega
wana changamoto nyingi sana. Kwamba wakulima wa pamba walipewa madawa
feki ya kuua wadudu, michango ya hovyo hovyo ni mingi mno na unyanyasi
wa wana-CHADEMA ni mkubwa vijijini.
Tanzania Daima
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment