Muuguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Yasinta Thomas,
amenusurika kushambuliwa na wananchi wakati akimhudumia binti wa miaka
15 (jina linahifadhiwa), aliyekuwa mjamzito wa miezi sita na kisha
kujifungua kabla ya muda watoto mapacha waliokufa.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Fredrick Mlekwa, jana
alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni wakati binti huyo
alipofikishwa hospitali hapo akitokea katika Kituo cha Afya cha
Kambarage, mjini Shinyanga.
“Tulimfanyia uchunguzi na kugundua alikuwa na mimba ya mapacha
lakini wakiwa tayari wamefia tumboni, hivyo muuguzi wa zamu katika wodi
ya wazazi alianza kumhudumia ili kuwatoa watoto hao tumboni” alisema.
Alisema wakati muuguzi wa zamu akiendelea na zoezi hilo, mama mzazi
wa binti huyo aliingia chumba cha kuzalishia na kumkuta mwanae
ametolewa viumbe mfu na kuanza kupiga kelele na kumfokea muuguzi huyo
kwa matusi hali iliyosababisha vurugu na wananchi kujaa kutaka
kumshambulia muuguzi huyo kwa madai amesababisha vifo vya mapacha hao.
Mlekwa alisema watoto hao walikuwa na uzito wa gramu 200 na 500 na
ujauzito huo wa miezi sita uliharibika mapema na kulazimika kuwatoa
watoto hao kwa upasuaji mdogo ili kuokoa maisha ya binti huyo.
Mama mzazi wa binti huyo, Mwanahamisi Juma, mkazi wa mtaa wa
Mshikamano mjini Shinyanga, alisema mwanaye ambaye ni mwanafunzi wa
kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwasele, mjini humo,
alishindwa kuhudumiwa kutokana na muuguzi huyo kuonekana bize akichati
na simu.
“Nilipoingia katika chumba cha kuzalishia nilimkuta mwanangu
anajifungua watoto hao huku muuguzi akichati na simu na kutompa msaada
wowote unaohitajika, hivyo kuamua kumfokea kwa hasira,” alisema
Mwanahamisi.
Hata hivyo, muuguzi huyo, Yasinta, alisema wakati binti huyo
anajifungua watoto walikuwa tayari wamekufa hivyo aliamua kuwapigia
wenzake simu ili wamsaidie na ghafla alivamiwa na mama huyo na kuanza
kuporomoshewa matusi hadi Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo alipoingilia
kati na kuokoa.
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment