Wataalamu wa afya wameonya kuhusu matumizi holela ya mafuta yanayopakwa mwilini kama dawa za kuzuia mbu, kwa kuwa zinaweza kuwa na madhara kwa baadhi ya watumiaji.
Kwa nyakati tofauti wataalamu hao wa masuala ya afya wamesema dawa
hizo ambazo zimekuwa zikitumika kupaka mwilini kama mafuta na matumizi
yake kuongezeka zaidi wakati huu kutokana na tishio la homa ya Dengue,
zinaweza kuwa na madhara kwa sababu mbalimbali.
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa Homa ya dengue
katika Hospitali ya Mwananyamala, Mrisho Rupinda alisema jana kwamba
watumiaji wanapoona madhara ya aina yoyote wanatakiwa kuchukua hadhari
hasa kwa wenye mzio (alerge).
Alisema kwa kuwa dawa hizo ni kemikali zinahitaji utaratibu na kwa
watoto inahitaji uangalifu mkubwa ambapo ni vyema kuwavalisha nguo ndefu
na iwapo kuna mbu wengi dawa hizo ni vyema zikapakwa juu ya nguo.
Alisema kwa kuwa ngozi za watoto bado ni changa na laini si vyema
kutumia dawa hizo moja kwa moja kwani zimetengenezwa kwa kemikali
zinazoweza kuwa siyo salama kwa ngozi za watoto.
![medisoft](https://lh3.googleusercontent.com/blogger_img_proxy/AEn0k_s7Fr80lf2jLEIX-I_pW9O2rXA4s9nLjitvtcmp39_0IIu3wkokGowU_3Mc50hBiPDNZ-hwe8XFbPD24MMzTlnHRYMTN-hCgO4hu7d-bvLSC0HwNdE56xGkjymC1np15UzGCxTPOQ=s0-d)
Alisema wenye vidonda wanatakiwa kujihadhari kwa kuhakikisha dawa
hizo hazigusi vidonda au sehemu zenye michubuko na inapobidi wapake juu
ya nguo, kwa wanawake wavaa nguo fupi ameshauri kuvaa soksi kisha kupaka
dawa hiyo juu yake kwa kuwa si lazima iguse ngozi.
“Madhara yanaweza kutokea kwa baadhi ya watu hasa wenye alerge (mzio)
na wenye matatizo ya ngozi, ni vyema kuchukua tahadhari. Madhara
yanaweza kutokea kwa yeyote na wakati wowote,” alisema Dk Rupita.
Mtaalamu wa afya ambaye ni Ofisa wa Taaluma na Udhibiti wa Magonjwa
wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Grace Saguti ameonya matumizi
yasiyo sahihi ya dawa hizo za kuzuia mbu mwilini na kusema watumiaji
wanatakiwa kupaka kwa kufuata taratibu na si kutumia kiholela.
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Dk. Saguti alisema
japokuwa suala hili ni la kitaalamu zaidi watu wanapaswa kuwa makini
kuhusu namna wanavyotumia vizuizi hivyo vya mbu katika miili yao.
“Vizuizi hivyo vinaweza kuwa na
reaction kutokana na mwili wa mtu. Sitalizungumzia kwa undani zaidi kwa
kuwa kila kitu kina madhara yake lakini watu wasikimbilie kutumia dawa
hizo bila kupata ushauri. Ninajua iwapo mtu atakuwa na vidonda si vyema
kutumia dawa hizo bila kufuata maelekezo kwa usahihi,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Saguti, suala hilo la matumizi linahitaji pia
tahadhari na kufuata maelekezo ikiwamo kuhakikisha mwili unakuwa safi
wakati wa kupaka dawa hizo ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza
kwenye ngozi.
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment