Aliyekuwa Miss Tanzania, Sitti Mtemvu.PICHA|MAKTABA Dar es Salaam/ Arusha.
Kashfa
ya aliyekuwa Miss Tanzania, Sitti Mtemvu imechukua sura mpya baada ya
Wakala wa Uzazi, Vifo na Ufilisi (Rita) kusema kuwa wamekamilisha
upekuzi wa taarifa alizotumia kuombea cheti cha kuzaliwa na vielelezo
hivyo vimelekwa polisi vikafanyiwe kazi.
Wakizungumza
na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, Ofisa mtendaji mkuu wa Rita,
Phillip Saliboko na Meneja masoko na mawasiliano, Josephat Kimaro
walisema upekuzi wa nyaraka zilizotumiwa na Sitti uliofanywa na
wanasheria wao, tayari umekamilika.
“Kazi
yetu (Rita) tumeimaliza na upekuzi wa taarifa za Sitti umekamilika na
kinachofuata sasa ni kupeleka nyaraka hizo kwenye mamlaka inayohusika
ambayo ni polisi, wao ndio wataamua nini cha kufanya,” alisema Kimaro.
Alisema
Rita haiwezi kumhukumu moja kwa moja mrembo huyo kuwa alighushi nyaraka
na kudanganya ili apate cheti hicho cha kuzaliwa kilichotolewa na Rita
Septemba na badala yake wanapeleka vielelezo walivyonavyo polisi ili nao
wavifanyie kazi.
“Sisi
(Rita) jukumu letu lilikuwa ni upekuzi wa nyaraka, kazi ambayo
imefanywa kwa ustadi mkubwa na jopo la wanasheria wetu na hadi sasa
imekamilika na kinachofuata ni kuzipeleka nyaraka hizo polisi ambao wao
ndiyo wenye jukumu la uchunguzi na kumchukulia hatua Sitti au la,”
alisema.
Wakati
huohuo, Saliboko akieleza kuwa bado wana changamoto ya baadhi ya watu
kudanganya taarifa zao ili wapate vyeti vya kuzaliwa na kusisitiza kuwa
wanaandaa mfumo maalumu ili kukomesha udanganyifu huo.
“Tukibaini
mtu ametumia udanganyifu ili kupata cheti, kwanza huwa tunamfutia cheti
chake na taratibu nyingine za kisheria zinafuata. Tunafanya hivyo kwa
watu wote wanaokuja kuomba vyeti kwetu na siyo kwa Miss Tanzania peke
yake japo hili la Sitti tunaiachia mamlaka husika ifanye kazi yake,”
alisema.
Sitti
Mtemvu aliingia kwenye kashfa ya kudanganya umri wake na nyaraka zake
mbalimbali zilionyesha alizaliwa 1989, umri ambao umepitiliza ule
unaotakiwa kwa mshiriki wa mashindano ya Miss Tanzania, huku cheti chake
kikionyesha alizaliwa 1991, hivyo kulazimika kuvua taji hilo.
Wakati
huohuo, mrembo aliyevikwa taji la Miss Tanzania nambari mbili, Lilian
Kamazima anatarajiwa kuwasili leo mjini Arusha na kupokewa kwa shangwe
akiwa na taji lake.
Taarifa
iliyotolewa na mkurugenzi wa Kampuni ya Mwandago Entertainment Ltd,
Faustine Mwandago iliyosimamia ushindi wake ngazi ya kanda ilisema kuwa
mrembo huyo atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(Kia) saa 6:00 mchana.
Mwandago
alisema kuwa mrembo huyo atapokelewa na wenyeji wake, wakiwamo wazazi
wake na kisha kupanda gari la wazi ili kuwapa fursa wakazi wa Arusha
kumshuhudia.
Alisema
kuwa mara baada ya kuwasili Arusha atapelekwa moja kwa moja nyumbani
kwao, Sakina ili kushiriki hafla aliyoandaliwa na wazazi wake pamoja na
ndugu, jamaa na marafiki.
Wakazi
wa Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi kumpokea mrembo huyo kwa
lengo la kumpa moyo na kulikaribisha taji hilo mara baada ya ukame wa
muda mrefu wa kupata taji la Miss Tanzania.
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment