Hakufai. Pengine ni neno linaloweza kuwakilisha uhalisi wa hali ilivyo katika baadhi ya hospitali kadhaa za Serikali nchini, ambako mamia ya wagonjwa wanateseka kutokana na uhaba wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambao umeendelea kuzikumba.
Wengi wa
wagonjwa waliohojiwa wanalalamikia kushindwa kumudu gharama za dawa
ambazo wanapaswa kuzinunua kwenye maduka wakisema hali hiyo inazifanya
afya za Watanzania wengi wenye kipato cha chini wanaozitegemea kuwa
shakani.
Uchunguzi umebaini kuwa uhaba huo pia umesababisha hospitali
nyingi kuwabana wagonjwa kwa kuwatoza fedha kwa ajili ya huduma, ili
kujijengea uwezo wa kununua dawa chache, pamoja na vifaa tiba kwa ajili
ya dharura.
Kwa jumla, hali ilivyo ni tofauti ya
matarajio ya wengi kwamba kungekuwa na mabadiliko, hasa baada ya
Serikali kutangaza kwamba imekwishalipa sehemu kubwa ya deni ililokuwa
ikidaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Hivi karibuni
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema wizara yake
imeilipa MSD Sh20 bilioni ili kupunguza makali ya uhaba wa dawa. MSD
inaidai wizara hiyo zaidi ya Sh90bilioni za ununuzi wa dawa, vifaa tiba
na vitendanishi.
Jana, Msemaji wa Wizara ya Afya,
Nsachris Mwamwaja alisema: “Siwezi kuzungumza chochote kwa sababu tayari
waziri wangu alishatoa tamko bungeni, kwa hiyo kauli yetu ndiyo
hiyohiyo aliyotoa mheshimiwa waziri.”
Sura halisi ya
uhaba wa dawa inaonekana katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI)
na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako hali imeendelea kuwa mbaya
kwani ukosefu huo wa dawa umesababisha baadhi ya wagonjwa kuzidiwa na
wengine kupoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu.
Hospitalini
Ocean Road, mwandishi wetu alikutana na mkazi wa Arusha, Ashura Iddi
aliyefika kutibiwa na kufuatana naye hadi katika duka alikokwenda
kununua dawa alizoandikiwa.
Akisaidiwa na mwandishi
huyo, Ashura ambaye amekatwa mkono wake wa kushoto kutokana na saratani
ya mkono iliyosambaa hadi kifuani, aliambiwa na mfamasia katika Duka la
Biomed lililo karibu na ORCI kuwa dawa zake za mionzi zinagharimu
Sh166,000.
Hata hivyo, mgonjwa huyo ambaye alikuwa
akikohoa mfululizo kiasi cha kutapika, hakuweza kununua dozi hiyo kwani
hakuwa na fedha hivyo kurudi wodini kuendelea kukaa akisubiri siku dawa
zitakapofika au kupata fedha.
Ashura amelazwa ORCI
tangu Oktoba 27, mwaka huu na anasema hajapata matibabu zaidi ya kupewa
dawa za maumivu aina ya diclofenac. “Nimekosa hata dawa ya allergy
(mzio) ambayo inauzwa Sh1,000 nimeambiwa hakuna,” alisema Ashura.
Kaimu
Mkurugenzi wa ORCI, Dk Diwani Msemo alisema bado hawajajua iwapo fedha
zilizotolewa na Serikali kupunguza makali ya uhaba wa dawa zitasaidia
kwa kuwa tatizo ni kubwa.
Mfamasia katika duka la dawa
la Biomed, Hilal Shamshudin alisema siku wagonjwa kati ya 20 hadi 50
hufika katika duka hilo kununua dawa za mionzi.
Alisema
hata baadhi ya madaktari nao hufika kununua dawa hizo kwa ajili ya
wagonjwa ambao pengine huwapa fedha wawasaidie kuzitafuta.
Mfamasia
huyo alisema dawa za mionzi ni ghali kwani wapo wagonjwa wenye dozi
kubwa ambao hutakiwa kununua dozi ambazo gharama zake ni kati ya Sh3 na
4milioni.
Mwanamke mwingine, Saumu Mfyonsi ambaye alikuwa akisumbuliwa na saratani ya utumbo, alifariki jana kutokana na kukosa dawa.
Ndugu
wa Saumu, Abdallah Mfyonsi alisema waliandikiwa dawa za zaidi ya Sh2
milioni lakini wakati wakizitafuta ndugu yao alifariki. “Wote huu ni
umaskini,” alisema Mfyonsi huku akibubujikwa na machozi.
Neema maduka ya dawa
Maduka
mengi ya dawa yaliyojengwa pembezoni mwa hospitali hizo za umma,
yananeemeka kwa kupata wateja wengi ambao kila wanapoandikiwa dawa na
madaktari hulazimika kwenda kuzinunua nje ya hospitali husika.
Katika
maduka ya dawa yaliyopo mbele ya lango la kuingilia katika Hospitali ya
Manispaa ya Temeke, baadhi ya wafamasia wake waliwaambia waandishi wetu
kwamba dawa zinazoongoza kwa kuwa na wateja ni zile zinazohusishwa na
kina mama wajawazito na uzazi.
Katika orodha ya dawa
zinazonunuliwa kwa wingi pia zimo za kutibu malaria, shinikizo la damu
na kisukari. “Hapa pia tunauza kwa wingi, vifaa tiba kama mipira kwa
wagonjwa waliofanyiwa upasuaji (wa kupitishia mkojo) ambao hutumiwa na
wanawake na wanaume,” alisema mmoja wa wafamasia.
Waandishi
walishuhudia mwanamume aliyeingia katika duka hilo na kununua mpira wa
mkojo wenye urefu wa mita 21, kwa ajili ya mgonjwa wake aliyelazwa
wodini.
Wakati hayo yakitokea, uchunguzi wetu ulibaini kuwa kuna uhaba mkubwa wa dawa katika hospitali hiyo ya Temeke.
Chanzo
chetu ndani ya hospitali hiyo kilisema hali ya dawa ni mbaya na hakuna
hata dawa za kutuliza maumivu, hivyo msaada wa haraka unahitajika wakati
wakiendelea kusubiri mgawo kutoka MSD.
Chanzo hicho
kilieleza kwamba kwa sasa madaktari wanalazimika kuwaandikia wagonjwa
dawa ili waende kununua katika maduka yaliyopo nje.
“Kwa
sasa stoo yetu ya dawa haina kitu, kiasi kidogo kilichopo kina dawa
chache ambazo haziwezi kukidhi mahitaji ya wagonjwa wanaofika hapa.
Zaidi, tuna upungufu mkubwa wa vifaatiba muhimu ambavyo pia wagonjwa
wanalazimika kwenda kuvinunua nje ya hospitali,” alisema ofisa mmoja
ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
Alisema dawa muhimu
zinazohitajika kwa sasa ni pamoja na amocyllin, ciprofloxcan,
diclofenac, diclofenac injection, cannular, misoprosol (kuzuia utokwaji
wa damu kwa wajawazito), multivitamin, albendazol na mobendazole.
Baadhi
ya vifaa tiba muhimu vilivyopelea ni pamoja na mipira ya kutolea mkojo
kwa wagonjwa, (catheter), namba 16 na 18 , kifaa cha kuchomea
sindano(cannular), mipira ya mikono na vitendanishi.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, hakuwepo hospitali jana na alipopigiwa simu, iliita bila majibu.
Muhimbili Vifo Nje nje
Katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Wodi za Sewa Haji na Kibasila
zimefurika wagonjwa hadi kwenye veranda na milango ya wodi hizo kutokana
na wagonjwa wanaotokana na ajali.
Msemaji wa Taasisi
ya Mifupa ya Hospitali Muhimbili (Moi), Almasy Jumaa alisema zaidi ya
asilimia 60 wamepata ajali za bodaboda na bajaji.
“Wodi
hizo zina uwezo wa kulaza wagonjwa kwenye vitanda 30 kila moja, lakini
sasa idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka hadi mara tatu ya uwezo wa
wodi na sisi hatuwezi kukataa kuwapokea, kwa hiyo pamoja na matatizo
mengine, tunawapokea na kuwalaza ndiyo maana unaona wamejaa kiasi
hicho,” alisema Almasy.
Mmoja wa wagonjwa, Elizabeth
Biligimana alisema tangu amelazwa na mgonjwa wake katika hospitali hiyo,
Aprili mwaka huu kwa ajili ya uchunguzi wa tumbo kujaa, hajawahi kupata
dawa za bure.
“Mara nyingi naambiwa ninunue baadhi na
baadhi napata huko ndani, ukiniuliza kuhusu kununua dawa naona kama
unatonesha vidonda vyangu,” alisema Biligimana.
Almasy
alisema japokuwa hawezi kuelezea kwa kina tatizo lililopo, lakini uhaba
wa dawa umekuwa kikwazo cha utoaji wa huduma katika viwango
vinavyotakiwa kwa kuwa wagonjwa wanalazimika kuandikiwa kutafuta dawa
nje ya hospitali.
“Kwa kiasi fulani utaratibu wa
uchangiaji ambao wagonjwa wanatakiwa kuchangia huduma ndiyo ambao
umekuwa ukitusaidia angalau kupata fedha kidogo kwa ajili ya kupata dawa
za kusaidia kunusuru hali,” alisema.
Hata hivyo,
kuhusu kiwango cha uhaba na hatua zinazochukuliwa, alisema hawezi
kulizungumzia hilo kwa kuwa tayari Waziri wa Afya alishatoa tamko na
kueleza kwamba Serikali imeshatoa fedha kwa MSD kwa ajili ya kulipa
madeni yake na kusambaza dawa katika hospitali zote za Serikali.
Imeandikwa na Florence Majani, Andrew Msechu na Kalunde Jamal-Mwananchi
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment