
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John
Mnyika, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kuunusuru mchakato wa Katiba Mpya
kwa kulivunja Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea Dodoma.
Aidha, amemtaka Rais kuitisha Bunge la kawaida ili uchaguzi mkuu mwakani uwe huru na haki.
Mnyika
alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya
kuwajengea uwezo vijana wa vyama rafiki wa Chadema lengo likiwa ni
kuwaandaa kwenye masuala ya uongozi. Mafunzo hayo ambayo ni mwendelezo
wa yale ambayo hutolewa na Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (DUA),
safari hii yamehusisha vijana kutoka Kenya, Uganda na Tanzania.
Akizungumza
kwenye mafunzo hayo, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema
vijana wa Tanzania na Uganda wanatakiwa kujifunza kutoka Kenya ambao
waliingia kwenye machafuko baada ya kufanya Uchaguzi Mkuu kabla ya
kupata Katiba Mpya.
Alisema
matokeo yake viongozi wake wa juu walifikishwa katika Mahakama ya
Kimataifa ya Uhalifu, (ICC). Alisema Kikwete anatakiwa atoke kwenye
siasa na kuvaa nafasi ya kiongozi ili kunusuru hayo yaliyotokea Kenya
yasijitokeze hapa.
Kuhusu
vijana wa nchi za Afrika Mashariki, Mnyika alitaja changamoto
inayowakabili kuwa ni ajira ambayo aliwataka waliobahatika kupata
mafunzo hayo, watoke na mkakati wa kufanya kampeni ya kupunguza tatizo
hilo.
Aliigusia
nchi ya Libya na nyingine duniani ambazo zinapigana vita huku akisema
moja ya sababu ya machafuko ni pamoja na ukosefu wa ajira.
Mwenyekiti
wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA),
Patrobass Katambi, alisema wanataka katiba inayokubaliwa na Watanzania
wote ambayo itakuwa na tija kwao.
Kuhusu
maandamano ya Chadema yanayoendelea nchini huku jeshi la polisi
likiyazuia kwa kuwakamata, mwenyekiti huyo alisema matendo ya chama
tawala ya kutumia dola vibaya ndiyo yanayosababisha vurugu na kutokea
vita.
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment