
Uamuzi huo ulifikiwa bungeni Mjini Dodoma, baada
ya wajumbe wa Bunge hilo kupitisha azimio la kuzifanyia marekebisho
kanuni ya 30, 36 na 38 za Bunge hilo za mwaka 2014.
Hata hivyo, wajumbe watatu kati ya 15 waliochangia
azimio hilo, walipinga vikali marekebisho hayo, lakini yalipitishwa kwa
wingi wa kura baada ya Mwenyekiti, Samuel Sitta kulihoji Bunge.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa raia wa Tanzania
kupiga kura akiwa nje ya nchi, uamuzi ambao Sitta aliutetea akisema
wanaoupinga wanachanganya kati ya kura ya uamuzi na kura ya uchaguzi.
Mwakilishi wa walimu, Ezekiah Oluoch alisema
Kifungu cha 16 (6) cha Kanuni za Bunge kinamtaka mwenyekiti kuendesha
Bunge kwa mujibu wa sheria walizonazo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na
sheria nyingine za nchi.
“Hoja ya walioko nje ya Bunge hili kupiga kura,
siiungi mkono na wengi mkiunga mkono mtakuwa mmekiuka sheria ... kila
raia ana haki ya kupiga, Katiba yetu inaeleza, ilimradi atimize miaka 18
lakini haki hiyo imewekewa pia utaratibu wa kisheria,” alisema.
Alisema kwa taratibu zilizowekwa nchini, hakuna unaomruhusu mtu aliyeko nje ya eneo la kupiga kura kufanya hivyo.
Hata hivyo, Sitta aliingilia kati akisema mjumbe
anasema uongo, akimtaka aeleze ni kura ipi anayoizungumzia na kifungu
gani kimesema hilo, naye akajibu kura anazozungumzia ni zote ikiwamo ya
kufanya uamuzi ndani ya Bunge.
“Unasema uongo mtupu wewe ... sheria ya uchaguzi,
tunamchagua nani hapa?” alihamaki Sitta na hali kama hiyo aliionyesha
pia kwa wajumbe wengine waliokuwa wakipinga marekebisho hayo.
Oluoch alisema anachoona ni kuwa si halali kwa
mjumbe ambaye hayuko ndani ya Bunge kupiga kura na kutaka Bunge
lisifanye mambo kwa sababu linataka kutimiza mambo ambayo si msingi wa
sheria.
“Uamuzi wowote huo tunaotaka kufanya kwa lengo la
kupata utashi wa kisiasa, mimi nitasimama peke yangu kukataa na itaingia
kwenye hansard (kumbukumbu za Bunge) kwamba nilikataa jambo hili,”
alisema.
Kwa upande wake, Said Arfi alisema hakubaliani na
azimio hilo kwa sababu Kanuni ya 38 ilikuwa imeshaweka utaratibu na
haoni kuwapo haja ya kufanya marekebisho.
“Jambo hili tunalofanya ni kubwa sana, kuandika Katiba ya Taifa
letu ni lazima tuwe na nia zilizokuwa njema ili kulipatia Taifa Katiba
ambayo itaridhiwa na Watanzania. Sioni sababu zozote za msingi kwa
wajumbe ambao hawapo humu ndani kupiga kura.”
Arfi alisema uzoefu wa mabunge mengi duniani
wanaopiga kura ni watu waliomo ndani ya ukumbi wa Bunge tu... “Sasa hii
ya kwenda kuwatafuta watu huko waliko hauna uhakika anayepiga kura
ndiye, ni shaka tupu. Kwa kweli mheshimiwa mwenyekiti Watanzania
watatutazama juu ya nia zetu na dhamira zetu juu ya kulipatia Taifa
Katiba maridhawa,” alisema.
Alisema kura ni hiari na mjumbe anaweza kuwapo
ndani ya Ukumbi wa Bunge na kuacha kupiga kura na kuonya kuwa
kuwalazimisha na kuwatafuta watu ili wapige kura si jambo la
kidemokrasia.
Wakati akiendelea, Sitta aliingilia kati na kumhoji nani anayelazimisha mtu kupiga kura? Arfi akamjibu;
“Unapotuingilia katika michango yetu Watanzania wanakupima. Watanzania wanakuheshimu mwenyekiti.”
Kwa upande wake, Ali Omary Juma alisema Katiba ni
maridhiano ya nchi mbili huru na si busara kuharakisha kupiga kura kwa
watu ambao hawamo ndani ya Bunge.
Alisema kama hilo litaruhusiwa itakuwa ni mgongano
mkubwa wa kisheria ambao utaleta ufa mkubwa kama uliojitokeza baina yao
na Ukawa … “Nashauri suala la kura tulisitishe ili kutoa fursa pana ya
mashauriano na kutoa muda ili wajumbe wote tuhudhurie.”
Mjumbe Paul Makonda aliunga mkono hoja hiyo akisema wajumbe zaidi 600 kuwa mahali pamoja si jambo rahisi:
“Nakumbuka tukiwa kwenye kamati yetu siku moja mtu
alilazimika kutoka hospitalini. Ni mgonjwa lakini afanyeje, lakini kama
kuna uhuru wa kupiga kura pale alipolala ni jambo la heri.
“Hatutafuti kura mpya. Hapa tunatafuta kupiga kura
kwa wale watu ambao walishajadili jambo hili, haina maana tunatafuta
kuokotaokota kama tumepungukiwa, hatujapungukiwa hata kidogo.”
Baadaye Sitta alisimama na kusema ipo dhana
inayojengeka kwamba utaratibu huo unalenga kulazimisha kila mjumbe
kupiga kura ili tu theluthi mbili ipatikane, hivyo akataka wajumbe
waache kupoteza muda ... “Hii ni dhana ya ajabu na ina nia mbaya ndani
yake. Mmoja wa watu ambao ameomba apige kura yuko hospitali India, nina
mamlaka gani ya kumkatalia?”
“Tumempigia Balozi atamwapisha atapiga kura ya
siri italetwa na itafunguliwa humu. Zote hizo zitafunguliwa humuhumu
ndani ya ukumbi na majina yatasomwa,” alisema Sitta.
“Watakaopiga kura mbele ya mabalozi wetu kwa wazi, Record
(kumbukumbu) yote italetwa hapa na mtashuhudia hapa majina yatatajwa
moja moja kama kanuni zinavyotaka,” alisema Sitta na kuongeza;
“Mambo haya ni ridhaa ya mtu, hakuna mtu
atalazimishwa. Kama kuna hao wanasimama hapa wanasema wanalazimishwa,
kama wameshindwa kuchangia hoja hii wasipoteze muda.”
Akijibu hoja za wajumbe, Mwenyekiti wa Kamati ya
Kanuni, Pandu Ameir Kificho alisema wakati wa kuhakiki mjumbe halali,
wale walioko watawasilisha pasi za kusafiria.
Wasomi wapinga
Akizungumzia uamuzi huo, Profesa wa Chuo Kikuu cha
Ruaha, Gaudence Mpangala alisema uamuzi huo ni dalili za kupaparika kwa
sababu kila kona Watanzania wanapinga kuendelea kwa vikao vya Bunge
hilo.
“Tanzania hatujafikia hatua ya kuruhusu wananchi
wapige kura wakiwa nje ya nchi yao, iweje leo tukubali jambo hili
kirahisi namna hii, kuna nini nyuma yake? Wanachokifanya bungeni
wananchi wanakifuatilia na watambue wazi kuwa hiyo Katiba
watakayoipitisha itapingwa.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), Dk Benson Bana alisema, “Kama wamekubaliana kubadili kanuni
sawa, ila lazima tujiulize kwa nini sasa. Kwa nini wabadili kanuni hizi
ili kupiga kura tu?”
Dk Bana alisema hakuna ulazima wa kuharakisha mambo ili kupata Katiba Mpya kutokana na hali halisi iliyopo sasa.
“Nasubiri kwa hamu kuiona hiyo Rasimu wanayotaka
kuipigia kura ili niilinganishe na iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Kuanzia hapo tutaanza kuhoji kama mambo yatakuwa tofauti,”
alisema.
Mwalimu wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu UDSM,
Faraja Christoms alisema sheria za nchi zinatakiwa kwenda sambamba na
Katiba ambayo ni sheria mama, hivyo kuruhusu upigaji wa kura wa aina
hiyo ni kinyume na sheria.
Aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS), Felix Kibodya alisema, “Unaweza ukabadili kanuni lakini haitakuwa
na maana kama hakutakuwa na maridhiano.”
Imeandikwa na Daniel Mjema, Sharon Sauwa na Fidelis Butahe wa gazeti la Mwananchi
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment