Polisi wamefanikiwa kumnasa mwanamke anayedaiwa kumtesa kwa
kipigo na kumng’ata mtoto Merina Mathayo (15), kumsababishia majeraha
makubwa kichwani.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura
akizungumza na Mwananchi jana alisema walifanikiwa kumnasa juzi,
mwanamke huyo akiwa mafichoni Mbagala wilayani Temeke.
“Tumefanikiwa kumnasa juzi usiku akiwa mafichoni kwa jamaa zake,
ni mwanasheria wa kujitegemea ana umri wa miaka 44, lakini inashangaza
kwa hayo aliyoyatenda, anaendelea kuhojiwa wiki ijayo tunatarajia
kumpandisha kizimbani,” alisema Wambura.
Mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa Boko, anadaiwa kumtesa mtoto huyo
ambaye ni mtumishi wake wa kazi za nyumbani, ambaye sasa amelazwa
katika wodi ya dharura ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa(MOI) Muhimbili Dar
es Salaam.
Wakati huo huo, Uongozi wa MOI umejizatiti kulinda usalama wa mtoto
huyo, kwa kuzuia vyakula kutoka nje ya taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na
kudhibiti watu kumtembelea na kuzungumza naye.
Mmoja wa wauguzi katika wodi aliyolazwa alieleza mtoto huyo kwa sasa anahudumiwa kila kitu na taasisi hiyo.
Ofisa Uhusiano wa MOI, Patric Mvungi , alieleza kwamba majibu ya
kipimo kikubwa cha CT Scan alichofanyiwa yametoka, ambapo yameonyesha
hakuna mfupa uliovunjika kichwani.
Mtoto Merina amelazwa Moi baada ya kupewa rufaa na Hospitali ya
Mwananyamala alipokuwa amelazwa awali, kutokana na majeraha hayo ya
kung’atwa meno na kupigwa na vitu mbalimbali.

Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment