Siku Diamond Platnumz anafagia tuzo saba za Kilimanjaro, ubavu wake wa kushoto Wema Sepetu alikuwa naye bega kwa bega. Na katika wakati mmoja alipanda jukwaani kutoa maneno ya shukrani kwa niaba yake na alisikika akisema anajivunia kuwa mke mtarajiwa wa staa huyo wa muziki nchini.
Wema na Diamond wana historia ndefu ya mapenzi na uhusiano wao
unaongoza kwa kuandikwa zaidi na vyombo vya habari pamoja na kuwa
midomoni kwa wapenzi wengi wa muziki nchini. Kwa pamoja, wana nguvu
kubwa ya ushawishi na kama kweli wakifikia lengo la kuwa mke na mume,
wana mustakali mzuri hapo baadaye.
Tunafahamu jinsi Diamond anavyopigana kujitanua kimataifa na bahati
nzuri jitihada zake hazipotei. Mwaka huu peke yake, Diamond amefanikiwa
kufanya mambo makubwa kuliko msanii yeyote wa Tanzania. Kuanzia video
yake ya My Number One akiwa na Davido kushika nafasi ya kwanza kwenye
runinga kubwa duniani ikiwemo Trace TV, kutajwa kuwania vipengele viwili
kwenye tuzo za MTV Africa na sasa kutajwa kuwania BET Awards kwenye
kipengele cha Best International Act: Africa.
Kama mambo yakienda vizuri na wengi wakimpigia kura, anaweza kunyakua
tuzo moja kati ya hizo. Na ukiangalia, huo ndio kama mwanzo tu wa
mafanikio yake, mengi makubwa yanaashiria kumfungulia milango na kukwea
juu zaidi.
Lakini swali nililonalo kichwani ni je! Wema anautumia umaarufu na fursa aliyoipata mwandani wake kuimarisha kile anachokifanya pia?
Lakini swali nililonalo kichwani ni je! Wema anautumia umaarufu na fursa aliyoipata mwandani wake kuimarisha kile anachokifanya pia?
Wema ni muigizaji wa kike wa filamu mwenye mashabiki wengi zaidi
kuliko wote nchini. Na kwa wale waliokwisha tazama filamu zake,
watakubali kuwa si umaarufu wake tu unaozifanya filamu zake zipendwe,
bali ni kweli kipaji cha kuigiza anacho. Na pengine akiwa chini ya
muongozaji mzuri wa filamu, anaweza kufanya makubwa zaidi katika fani
hiyo.
Kinachomtofautisha na waigizaji wengine wa Tanzania, ni msingi wa
elimu alioupata na hivyo kuwa na kigezo muhimu wanachokosa waigizaji
wengine wa Tanzania ambacho ni uwezo wa kuongea Kiingereza vizuri.
Sijaona jitihada zozote ambazo mrembo huyu anazifanya kutumia jina la
mpenzi wake ambaye kwa sasa nchi nyingi za Afrika zinamfahamu
kutengeneza njia na kupata fursa ya kufanya filamu za kimataifa.
Ninachokiona akikifanya Wema kwa sasa, ni kuendelea kufanya kile kile
ambacho waigizaji wengine wa filamu wa Tanzania wanakifanya – kuigiza
filamu kwaajili ya soko la ndani. Haoni kuwa huu ni muda wa yeye kupiga
hatua moja pia?
Kuna wakati Wema alikuwa anataka kuelekea huko. Mwaka 2012
alifanikiwa kumdondosha muigizaji mkubwa wa filamu wa Nigeria, Omotola
Jalade kwenye uzinduzi wa filamu ya Supastaa ambayo hata hivyo
haikutoka. Huo ulikuwa mwanzo mzuri wa yeye kujitangaza kwenye filamu za
kimataifa kama ambavyo marehemu Kanumba alikuwa akikifanya kabla ya
mauti yake.
Nahisi njia nzuri ambayo Diamond angeweza kumsaidia Wema kufanikiwa
hilo ni kusafari naye mara kwa mara katika safari zake za kimataifa na
huko angekuwa anamuunganisha na wadau muhimu wa fani yake.
Kwakuwa kwa sasa tayari ana jina Nigeria, alikuwa anaweza kumweka
karibu na kiwanda cha Nollywood ambacho kwa Afrika ni kikubwa zaidi
kibiashara. Alikuwa na uwezo pia wa kumuunganisha na vyuo vizuri kwa
masomo ya filamu ambako huko angenoa zaidi uwezo wake wa kuigiza.
Kama wanapendana na lengo lao ni kuja kuwa pamoja, nahisi kuna wakati
wanahitaji kuanza kusafiri pamoja na hii inaweza kumfungulia Wema fursa
zaidi kuliko sasa ambapo anaonekana kuridhika na anachokifanya
nyumbani.
Credit: Bongo5
Credit: Bongo5
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment