Dodoma. Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amechaguliwa kwa kishindo kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba, huku akisema kuchaguliwa kwake ni sawa na kumrudisha chura kwenye dimbwi la maji.
Jana, Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alipata kura 487 na kumbwaga mpinzani
wake, Hashimu Rungwe wa Chama cha Ukombozi wa Umma aliyepata kura 69.
Wajumbe wengine, Dk. Terezya Huvisa pia wa CCM na John Chipaka wa
Tadea, walijitoa katika kinyang’anyiro hicho ambacho tangu awali Sitta
alionyesha kujiandaa kwa kutengeneza vipeperushi alivyovisambaza kwa
wajumbe kama sehemu ya kujinadi.
Akizungumza na wajumbe ambao muda mwingi walikuwa wakimshangilia,
Sitta alionekana kujiamini kabla na baada ya uchaguzi. Pia alitumia
misemo lugha ya picha ikiwamo ya chura kuishi majini, akimaanisha kuwa
wajumbe wamemchagua mtu mwenye uwezo, uzoefu na weledi wa kuongoza
shughuli za Bunge.

“Jamani kunichagua mimi ni kama kumrejesha chura kwenye dimbwi la
maji alilolizoea. Msiwe na wasiwasi ataogelea tu na ninawaahidi kuwa
ikiwa kwa kudra za Mwenyezi Mungu, mtanichagua nitawatumikia kwa
uaminifu, sitakubali upendeleo wa aina yoyote, nitasimamia kanuni
tulizozipitisha hapa,” alisema.
Aliongeza kusema: “Nitawaongoza kwa utumishi uliotukuka na uadilifu
ili tupate Katiba bora, yenye viwango na kwa wakati. Nina hulka ya
kuwapenda wale ninaowaongoza, kwa hiyo nitakuwa mtetezi wa shughuli
mbalimbali…Ninawaahidi Watanzania kutenda haki na kuwapatia Katiba yenye
viwango na kwa wakati.
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, Sitta alikuwa Spika wa Bunge la Tisa
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akiongozwa na falsafa yake ya Bunge
la kasi na viwango. Pia anatajwa kufanikiwa kuliongoza Bunge hilo kwa
weledi wa hali ya juu.
Kwa sababu ya mafanikio hayo, alipokuwa akiomba kura za wajumbe wa Bunge hilo, hakusita kujifananisha na chura kurudi majini.
Aidha, alisisitiza kuwa ataliongoza Bunge kwa kutumia falsafa yake
ya kasi na viwango, huku akiahidi kulisimamia Bunge kwa haki na bila
upendeleo kwa kundi lolote.
Matokeo ya kura
Akitangaza matokeo, Msimamizi wa Uchaguzi, Dk. Thomas Kashillilah,
alisema Sitta alipata kura hizo 487 ambazo ni sawa na asimilia 86.5,
kati ya kura 563 zilizopigwa.
Dk Kashillilah alisema kwamba mpinzani wa Sittta, Hashim Rungwe
ambaye jana tulimwandika kimakosa kuwa anatoka NCCR- Mageuzi alipata
kura 69, sawa na asilimia 12.3 ya kura zote. Alisema kura saba
ziliharibika.
Moja ya mambo yaliyovuta hisia za wajumbe wengi ni hatua ya Sitta
kushikana mikono ya kupongezana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
baada ya kumaliza kuomba kura kutoka kwa wajumbe.
Sitta na Chenge
Akitoa shukurani zake baada ya kuchaguliwa, Sitta alisema hana
uhasama wowote na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ambaye naye
awali alikuwa na nia ya kuwania nafasi hiyo kabla ya kujitoa.
“Namshukuru pia ndugu yangu Andrew Chenge ambaye watu walivumisha
kwamba tulikuwa na mchuano wa uhasama ndani ya chama, jambo ambalo siyo
kweli, “alisema na kuongeza;
“Mheshimiwa Andrew Chenge tuna historia ndefu sana, nikiwa Waziri
wa Katiba na Sheria mwaka 1993, mimi ndiye niliyependekeza jina kwa Rais
wa Awamu ya Pili, Rais Ali Hassan Mwinyi ili ateuliwe kuwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.” alisema.
Kwa upande wake, Chenge alisema: “Mambo yote yaliyozungumzwa na
Sitta ni mambo yaliyopita, kilichopo ni kutazama kazi iliyo mbele yetu.”
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment