0
kinnaa
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema licha ya mawaziri ‘mizigo’ kubaki kwenye Baraza la Mawaziri kinyume na mapendekezo yake, hatajiuzulu.
Kauli hiyo ya Kinana imekuja huku kukiwa na shinikizo kutoka pande mbalimbali kumtaka ajiuzulu kwa kile kilichoitwa kupuuzwa kwa mapendekezo ya Sekretarieti ya CCM anayoiongoza na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na Rai Kinana alisema: “Sote tumesikia uamuzi wa Mwenyekiti wetu Rais Kikwete, hatuwezi kupingana naye, lakini mapambano dhidi ya watendaji wabovu yanaendelea.
“Mtu unapokuwa vitani halafu ukishindwa katika hatua moja, unachopaswa kufanya ni kubadili mbinu za medani na kusonga mbele, kwa hiyo hatujakata tamaa.
“Tuliyoyasema na kuyajadili kwenye chama ni mapendekezo na maoni ya wananchi tuliyoyapata wakazi wa ziara yetu ndefu ya kuimarisha chama, hayakuwa yakwangu Kinana.
“Hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema tuhuma inatosha kabisa kumuondoa kiongozi madarakani, sasa baadhi ya tuhuma za mawaziri zilianza hata kabla ya sisi kwenda kwa wananchi.
“Kama Waziri Kawambwa, yeye baada ya matokeo mabaya ya Kidato cha Nne kuwahi kutokea nchini kwa watahiniwa wa mwaka 2012, wito wa kumtaka aachie ngazi ulisikika kila kona ya Tanzania.”
kinnaa
Katika sakata hilo la kufeli wanafunzi wengi, Februari mwaka jana, Dk. Kawambwa alitangaza matokeo ya Kidato cha Nne na kubainisha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndio waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 walipata Daraja la Nne.
Watahiniwa walikuwa 456,137 kati yao wa shule wakiwa 397,136, wa kujitegemea 68,806.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa waliopata Daraja la Kwanza walikuwa 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, Daraja la Pili 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1,997.
Matokeo hayo yaliibua mjadala mkali huku makundi mbalimbali ya jamii yakihoji sababu zilizosababisha wanafunzi wengi kufeli na kutaka Kawambwa na wasaidizi wake wawajibike, kabla Waziri Mkuu kuunda Tume iliyoongozwa na Profesa Sifuni Mchome kuchunguza, ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Kuhusu kujiuzulu, Kinana alisema katika kipindi ni vema kutoa nafasi kwa busara kufanya kazi, kwa sababu lengo kuu si kukidhoofisha au kuleta mpasuko ndani ya CCM.
“Nikisema nijiuzulu itakuwa ni sawa na kushiriki kuua chama, pia si busara kufikia hatua kama hiyo kwa sababu itakuwa kama kuanzisha mapambano na Mwenyekiti wetu,” alisema.
Baadhi ya mawaziri mizigo waliotajwa na CCM ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na aliyekuwa Naibu wake, Adam Malima, ambaye amekuwa Naibu Waziri wa Fedha.
Baada ya ziara ya Kinana mikoani kuwataja mawaziri hao mwishoni mwaka jana, wabunge 160 wa CCM walijiorodhesha kuomba kuitishwa kwa kikao cha Kamati ya Wabunge hao kwa lengo la kuwajadili mawaziri wanaotajwa kuwa mizigo.
Pia wabunge hao walimtaka Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahaman Kinana awepo kwenye kikao hicho.
Mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Hussein Mussa Mzee, alinukuliwa akisema walipokea barua iliyoambatana na orodha ya majina ya wabunge zaidi ya 160 waliotia saini kutaka kuitishwa kwa kikao hicho.
Baadae, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa akisema kuwa mawaziri saba walihojiwa katika kikao cha Kamati Kuu na kumuachia Rais Jakaya Kikwete jukumu la kuamua kuwafukuza kazi, kuwahamisha au kuwataka kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Tangu kuzuka kwa mjadala wa mawaziri ‘mizigo’ kumekuwapo na maoni tofauti kutoka kwa wananchi wakiwamo viongozi wastaafu wa CCM.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Mzee Yusuf Makamba alinukuliwa na vyombo vya habari akikosoa hatua ya Kinana kuwataja hadharani wamaziri hao.
Makamba alisema suala hilo lilipaswa kujadiliwa kwenye vikao vya chama, na kumtaka Rais Kikwete kutowaengua katika Baraza lake la mawaziri.
Pia Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa na mmoja wa waasisi wa chama hicho Mzee Peter Kisumo, kwa nyakati tofauti walisema ni makosa kuhoji uteuzi wa mawaziri unaofanywa na Rais, kwa sababu Katiba inampa mamlaka hayo yeye Rais pekee.

Post a Comment

toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment

 
Top

SOMA HABARI KEM KEM KUPITIA BLOG YAKO PENDWA YA HISIA ZA MWANANCHI HAPA

X