Pia kimewatahadharisha viongozi wa Chadema Kanda ya Ziwa kwamba yeyote atakayeonekana kuwa karibu na Zitto katika shughuli za chama au kutoa siri, atashughulikia haraka na kuwekwa kwenye kundi la wasaliti.
Akizungumza jijini hapa jana, Kiongozi wa Operesheni Kanda ya Ziwa Magharibi, Tungaraza Njugu, alisema kuwa wanaunga mkono kwa asilimia 100 uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema wa kuwavua uanachama Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, huku Zitto akipachikwa jina la ‘Mbunge wa Mahakama’.
Njugu alisema uamuzi huo ni sahihi kwani watu hao watatu waliaminiwa na chama, lakini wakakigeuka na kukisaliti kwa manufaa yao.
“Kwa kitendo alichokifanya, kukisaliti chama na kukipeleka Mahakamani, tunasema hatumtaki kabisa, ingawa ana haki ya kwenda sahemu yoyote na kufanya mkutano lakini tunatoa tahadhari mapema.
“Ikiwa atakuja Mwanza na kujihusisha au kutumia nembo ya chama katika shughuli zake za kisiasa, hapo atakuwa amechokoza nyuki. Hivyo hivyo kwa kiongozi atakayeonekana kuwa karibu au kumpa ushirikiano, atashughulikiwa haraka.
“Zitto hawezi kuwa kikwazo kwa Chadema kufikia malengo yake, tunasema chama hiki hakijabomoka wala kugawanyika makundi yenye mitazamo tofauti, hii ni kama hali ya baba kumwadhibi mtoto wake.
“Tunajua hizi vurugu zinazotokea zinaratibiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Usalama wa Taifa na vyama vingine vya siasa ambavyo vinatishwa na nguvu za Chadema. Lakini tunasema tutafika Ikulu salama,” alisema.
Njugu alisema kitendo cha Zitto kutoa tuhuma kwa viongozi wa Chadema ni dalili ya kuanza kutapatapa kutafuta huruma ya wananchi na Mahakama.
Alisema kama alikuwa anajua viongozi hao wana tuhuma za aina hiyo, angezitoa mapema kabla ya kuibuka yaliyompata.
“Unajua kuna wabunge ambao waliandaliwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe, tangu wakiwa vyuoni akiwamo Zitto. Amefika hapo kwa sababu ya Mwenyekiti sasa anakosa fadhila.
“Wengine ambao Mbowe alikuwa akiwaandaa wakiwa vyuoni ni John Mnyika, Halima Mdee, Ezekiel Wenje na John Mrema ambaye ni kiongozi mkubwa Makao Makuu.
“Mbowe alikuwa akiwafuata vyuoni na kukaa nao baada ya kuona ni vijana wenye mwelekeo wa kuleta mabadiliko na chama kikawaamini na hata kuwapa majimbo. Lakini naona Zito amejisahau.
“Mimi nawaomba viongozi wa kitaifa kutofanya kosa la kumsamehe au kumrejesha ndani ya chama pengine kutokana na uamuzi wa Mahakama. Itakuwa ajabu kweli kweli na wanachama hawataelewa,” alisema.
Wakati huo huo, makundi ya wanachama wa vyama mbalimbali walikusanyika eneo la Kemondo maarufu kama ‘Bunge la Mwanza’ kuzungumzia kinachoendelea ndani ya Chadema.
Eneo hilo ambalo lipo katikati ya jiji likiwa na matawi ya Chadema na CUF, wanachama wengi wa Chadema walipongeza hatua hiyo.
Wanachama hao walikuwa wakisoma magazeti mbalimbali kwa sauti kuhusu Zitto, na kujadiliana ambapo asilimia kubwa walionekana kutoridhishwa na mwenendo wa kada huyo wa Chadema.
Source: Rai
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment