WATUMIAJI wa simu wapatao milioni nane wapo
hatarini kufungiwa simu zao ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, Tanzania
Daima limebaini.
Tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeziandikia
kampuni za simu waraka wa kuzitaka zianze kukata kodi mpya ya laini
(simu card) mara moja kuanzia Julai 30, 2013.
Hatua
hiyo inatokana na serikali kushindwa kufuta kodi hiyo ya sh 1,000
iliyopitishwa na Bunge kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete baada ya
kukutana na wadau wa sekta ya mawasiliano.
Kwa
maana hiyo kila anayemiliki laini moja ya simu atakatwa sh 3,000;
anayemiliki laini mbili sh 6,000 na anayemiliki laini tatu sh 12,000,
lengo ni kuhakikisha serikali inakusanya sh bilioni 178 zitakazopelekwa
kwenye bajeti kuu ya serikali.
Watumiaji wa simu sasa watalazimika kulipia kodi hiyo ya
miezi mitatu ya Julai, Agosti na Septemba kwa wakati mmoja.
Bunge
kupitia Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi,
Andrew Chenge (CCM) lilitaka kuwapo kwa kodi hiyo ili kusaidia shughuli
za bajeti ya Serikali Kuu.
Kupitishwa kwa kodi hiyo kuliibua malalamiko ya wanasiasa
dhidi ya Chenge anayelazimisha kuwapo kwa kodi hiyo, huku akishindwa
kuamini kwamba kuna Mtanzania anayekosa sh 1,000 kwa mwezi kwa ajili ya
laini ya simu.
Malalamiko
hayo yaliendelea hadi kwa wananchi na baadhi ya wabunge wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliotaka posho za wabunge zipunguzwe
ili kuziba pengo hilo badala ya kuwabebesha wananchi mzigo.
Inadaiwa
kwamba msimamo wa Chenge unaungwa mkono na Spika wa Bunge, Anne
Makinda, jambo lililosababisha kutojadiliwa kwa hoja binafsi ya Mbunge
wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) iliyohusu kodi hiyo katika mkutano wa
Bunge lililopita kwa kisingizio cha kukosekana kwa muda wa kufanya
hivyo.
Hata
hivyo, takwimu zilizotolewa na kampuni za simu zinaonyesha kuwa miongoni
mwa wamiliki wa laini za simu milioni 22; milioni nane wanatumia chini
ya sh 1,000 kwa mwezi.
Baada ya malalamiko hayo, Rais Kikwete alikutana na wadau
wa mawasiliano ambao ni wamiliki wa kampuni za simu Tanzania (MOAT),
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na
Waziri wa Fedha, William Mgimwa, kisha kuwaagiza waiondoe kodi hiyo.
“Rais
alisema lengo kuu la mkutano huo liwe kupendekeza jinsi ya kuziba pengo
la sh bilioni 178 zitakazopotea katika bajeti iwapo kodi hiyo itafutwa.
“Alisema
hawezi kuifuta moja kwa moja kodi hiyo, bila kutafuta njia nyingine za
kupata fedha kujazia pengo litakalotokeza huku tayari Bunge limezipangia
matumizi,” alinukuliwa Makamba baada ya kikao hicho na rais.
Kwa
upande wake, rais alikaririwa akiwaambia wadau hao wa mawasiliano
kwamba: “Nakuombeni kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili
yenu pamoja tutafute namna gani tutajaza pengo hili la sh bilioni 178
endapo tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito, na
kuwa pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu.”
Licha ya
agizo hilo la rais kutekelezwa kwa MOAT kutakiwa kuongeza kodi nyingine
iitwayo ‘Excise duty’ kutoka asilimia 14 hadi 17 bila kujali kwamba
katika Bunge la bajeti kodi hiyo iliongezwa kutoka asilimia 12 hadi
asilimia 14, tozo hiyo ya laini za simu haijaondolewa.
Wachambuzi
wa masuala ya siasa na mawasiliano walisema kutojadiliwa kwa mabadiliko
ya kodi hiyo ya simu ni dalili kwamba Waziri wa Fedha amezidiwa nguvu
na kiti cha spika kinachounga mkono hoja hiyo ya Chenge na kushindwa
kutekeleza agizo la rais.
Wataalamu wa mawasiliano walilieleza gazeti hili kwamba
kuongezeka kwa kodi hiyo kutaifanya Tanzania kuwa na kiwango cha juu cha
kodi kuliko nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ushauri
wa wataalamu hao ulibainisha kwamba kuongezeka kwa kodi hiyo kunaleta
nafuu kidogo kuliko ile ya laini za simu inayomuumiza zaidi mwananchi wa
kawaida.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment