0

KIKUNDI cha waasi cha M23 kinachopambana na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kimeripotiwa kupigwa vibaya na kutikisa nguvu za kikundi hicho kutokana na baadhi ya wapiganaji wake kuripotiwa kupoteza maisha.
 
Mapigano baina ya M23 na Jeshi la Serikali ya DRC linalosaidiwa na Kikosi Maalumu cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO), yameibuka upya ndani ya wiki hii.
 
Habari za kiintelijensia  zinasema kuwa, kutokana na shambulio hilo, Serikali ya Rwanda imelazimika kuingilia kati kusaidia waasi hao kwa kupeleka bataliani mbili zenye jumla ya askari 1,700 huko DRC, ili waweze kukabiliana na nguvu ya majeshi ya JWTZ, DRC, Monusco na Brigedi ya Majeshi ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa yenye mamlaka ya kujibu mapigo (FIB).

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, Rwanda imepeleka bataliani hizo mbili zenye askari 850 kila moja saa 48 zilizopita na kwamba wamevuka mpaka kuingia DRC katika eneo la Kibumba, lakini wanashindwa kusonga mbele.
 
Habari zaidi zinasema sababu ya Rwanda kupeleka askari wake hao ni kusaidia M23 ambao walipigwa sana Agosti 23 na 27, mwaka huu katika eneo la vilima vya Kibati na  kuikimbia ngome yao.
 
“M23 walitandikwa sana Agosti 23 na 27 katika eneo la vilima vya Kibati, na kulazimika  kuikimbia ngome yao, ndio maana sasa hivi Rwanda imepeleka batalioni zao kuwapa nguvu, lakini wanashindwa kusonga mbele maana hawajielewi kwa sababu ya kipigo walichopata,” kilisema chanzo kimoja cha habari.
 
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, eneo la Kibati ndilo eneo kubwa la M23 ambalo wamekuwa wakitumia kuhifadhi silaha zao za kivita, lakini wakati wa mapambano majeshi ya JWTZ , DRC, MUNUSCO na FIB yalisambaratisha kabisa ngome hiyo ya waasi.
 
FIB inaundwa na askari wengi wa Afrika Kusini na Tanzania. Habari zaidi zinasema kwa sasa majeshi ya DRC, Monusco na FIB yanawasubiri kwa hamu askari hao wa Rwanda kuingia uwanja wa vita ili kukabiliana nao kama walivyokabiliana na waasi wa M23.
 
“Taarifa tulizonazo hivi sasa Rwanda inajiuliza iwapo isonge mbele kupambana au irudi nyuma, ikifikiria pia kipigo walichopata M23,” kilisema chanzo kimoja cha habari. 

Inaelezwa kwamba, kutokana na kipigo walichopata M23 siku chache zilizopita kimepelekea Rwanda kujikuta ikikiri na kusema ukweli juzi kuwa inakisaidia kikundi hicho cha waasi.

Post a Comment

toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment

 
Top

SOMA HABARI KEM KEM KUPITIA BLOG YAKO PENDWA YA HISIA ZA MWANANCHI HAPA

X