Hakimu wa
Mahakama ya Mwanzo iliyopo eneo la Nguzo Nane, Kata ya Kambarage Mjini
Shinyanga, Satto Nyangoha amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu katika shavu
lake la kushoto baada ya kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa baiskeli.
Kitendo hicho
kinadaiwa kufanywa na mlalamikaji katika kesi hiyo, Emmanuel Izengo
(28), mkazi wa Tambukareli, Shinyanga baada ya kutokuridhishwa na hukumu
iliyotolewa bila ya mshtakiwa, Daniel Makelezia, mkazi wa Lubaga
Shinyanga na mdhamini wake, Marko Nkelezia kuwepo mahakamani.
Katika hukumu
yake, Hakimu Nyangoha alisema mshtakiwa atakapopatikana atatumikia
kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa
baiskeli hiyo aina ya Neria yenye thamani ya Sh150,000.
Awali,
ilielezwa kwamba baada ya tukio hilo la wizi lililotokea Agosti Mosi,
mwaka huu katika eneo la Nguzo Nane, mshtakiwa alikamatwa na kuwekwa
mahabusu na kufunguliwa kesi namba 460 ya 2013 kabla ya kuachiwa kwa
dhamana Agosti 23, mwaka huu huku kesi yake ikiendelea na pande zote
mbili zilitoa maelezo.
Hata hivyo,
baada ya kutoa maelezo, si mshtakiwa wala mdhamini wake aliyehudhuria
mahakamani hapo licha ya kesi hiyo kusikilizwa mara mbili bila ya
taarifa yoyote kabla ya hakimu huyo kutoa hukumu hiyo jana.
Kushambuliwa
Baada ya
hukumu hiyo mlalamikaji alitoa shukrani na kuwashika mikono wote
waliokuwamo mahakamani humo na kutoka nje.
Ilidaiwa kuwa
baada ya dakika 15, Izengo alirudi mahakamani hapo na kudai kuwa ameleta
risiti ya kumwonyesha hakimu thamani ya baiskeli yake alipoingia ndani
ndipo kelele za Mshauri wa Baraza, Mary Wamba zikaanza kusikika akisema:
‘Njooni jamani hakimu kavamiwa anapigwa’.
Baada ya watu
waliokuwa karibu kuingia katika ofisi ya Mahakama hiyo walikuta hakimu
ameshacwhomwa kisu katika shavu la upande wa kushoto huku akivuja damu
nyingi huku mtuhumiwa huyo akiendelea kumshambulia. Baada ya tukio hilo,
wasamaria wema walimpeleka hakimu huyo katika Hospitali ya Mkoa wa
Shinyanga ambako alilazwa kwa matibabu.
Akizungumzia
tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema
mtuhumiwa alikamatwa mara baada ya tukio hilo kusubiri hatua za
kisheria dhidi yake.
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment