TAKRIBAN mwaka mmoja tangu alipoeleza aina ya jeneza atakalotaka
azikwe siku akifa, mwanamuziki Judith Wambura 'Jide' au 'Anaconda'
ameibua jingine jipya, safari hii ameandika wosia wa kifo chake, uchambuzi kamili.
ATIMIZA AHADI
Kama alivyoahidi mashabiki wake wiki moja iliyopita
kupitia mtandao wake wa kijamii, Jumatano ya Mei Mosi, mwaka huu,
mishale ya saa 8:00 mchana, Jide au Komando aliandika wosia huo wenye
maneno 555 akiwataja watu ambao asingetaka wafike kwenye msiba wake siku
akifariki dunia.
NI KWA WATANZANIA WOTE
Katika sentensi nyingine, mwanadada huyo
ameandika wosia huo kwa Watanzania wote watakaokuwa bado hawajatangulia
mbele ya haki yeye atakapofikwa na mauti.
ASIOTAKA WAFIKE
Katika wosia huo, Jide alitupa tuhuma nzito kwa
mabosi wa Clouds Media Group hasa Radio Clouds FM, Joseph Kusaga na Ruge
Mutahaba kuhusika katika kumhujumu kwenye tasnia ya muziki nchini huku
akiwataka wasifike kuaga maiti yake.
RADIO ISITANGAZE KIFO CHAKE
Katika kuupitia wosia huo, Ijumaa
limebaini kuwa, Jide alizuia Kituo cha Radio Clouds FM kisitangaze kifo
chake wala kupiga nyimbo zake siku atakapokufa.
AJITOA FIESTA, KISA?
Ndani ya wosia huo, mwanamuziki huyo
aliendelea kudai kuwa alijitoa kwenye shoo za Fiesta zinazofanyika kila
mwaka ambapo kwa mara ya mwisho alilipwa Sh. 800,000 na kuanzia hapo
ndipo fukuto la kubaniwa lilipoanza.
Alisema bifu likapamba moto
mwaka 2003 alipotoa albamu yake ya pili iliyojulikana kwa jina la Binti.
KISA? MACHOZI BAND
Aliandika kuwa tatizo lingine lililochochea
yeye kukandamizwa ni baada ya kuacha kufanya shoo za Clouds na kuanzisha
bendi yake ya Machozi ambapo alijiajiri mwenyewe na kupata mafanikio
jambo ambalo anadai jamaa hao hawakulipenda hivyo kuanza kuchochea mbinu
za ‘kumuua’ kisanii.
KUKANDAMIZWA
Aliwatuhumu kuwa kwa muda mrefu ‘wabaya’ wake hao
wamekuwa wakifanya njama za kumkandamiza ili kuhakikisha anapotea kabisa
kwenye muziki.
ASISHIRIKIANE NA WASANII WENGINE?
Alizidi kuandika kwamba watu hao
wamekuwa wakitishia kutopiga nyimbo zake alizoshirikishwa na wasanii
wengine wa Bongo.
FITINA
Jide aliandika: Nilinyamaza kwa muda mrefu lakini kadIri
muda ulivyosonga mbele ndivyo hali ilivyozidi kuwa mbaya kwani jamaa hao
waliongeza fitina kwangu kila kukicha.
VIKAO VINNE
Jide aliendelea kutuhumu kuwa jamaa hao hadi sasa
walishakaa vikao vinne vilivyolenga kumpoteza kabisa kwenye ramani ya
muziki huku akidai ni wafitini ambao wamekuwa wakipita kila mahali
kuhakikisha wanaziba mrija wa kumuingizia ‘chochote kitu’.
UPANDE WA PILI UNASEMAJE?
Baada ya kuutathimini wosia huo na kuona
ni kwa jinsi gani ulivyojaa tuhuma zilizohitaji majibu, kama kawaida ya
Ijumaa lililojaa weledi lilitafuta upande wa pili, Clouds Media Group
ili kupata majibu ya kile alichokiandika msanii huyo.
Mmoja wa mabosi
wa Clouds ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si
msemaji wa kampuni, pamoja na kukiri kuuona wosia huo, alichambua
kipengele kimoja baada ya kingine.
KUHUSU KUBANIWA
“Kama ana ushahidi ni lini alibaniwa aweke data
mezani. Unajua watu wametengeneza kizazi cha chuki bila kuwa na sababu
ya msingi.
“Hata msanii chipukizi akiibuka leo ataambiwa fulani
anabaniwa na kujikuta akijenga chuki bila kujua anayeeneza hayo ana
lengo gani.
“Ipo mifano ya wasanii wengi ambao nyimbo zao hazipigwi
katika vituo f’lanif’lani vya redio (akavitaja) kama Diamond na Juma
Nature, mbona huko hawapaoni wanaona Clouds pekee?”
KUHUSU KUKANDAMIZWA
“Kama kuna ushahidi ni lini aliandaa shoo au
aliitwa kwenye shoo then (halafu) watu wakamkandamiza kwenye malipo
auweke wazi, kwani hakuna mikataba? Ingekuwa ni vizuri akatoa mikataba
kuwa alikandamizwa kuliko kujenga chuki zisizokuwa na msingi. Anasema
alilipwa shilingi laki nane, kwa nini hakukataa? Kwani alilazimishwa?”
KUHUSU ASISHIRIKIANE NA WENZAKE
“Ukweli ni kwamba hatujawahi
kubana kupiga wimbo wa mtu kisa ameshirikishwa yeye. Hayo ni maneno
ambayo mwisho wa siku hawezi kuthibitisha kwa data.”
KUHUSU KUMFITINI
“Mtu amfitini ili apate faida gani? Kama hakuna
faida hakuna sababu ya kumfitini mtu katika biashara yake.”
VIKAO VINNE NA KIFO
“Hayo mengine ya vikao mimi siyajui na siwezi
kuzungumzia kifo cha mtu kwani huo ni wosia wake.”
KUNA KITU KIKUBWA KINAKUJA
Kwa mujibu wa bosi huyo, hali
inavyoendelea kuna kitu kikubwa kinakuja na ili kuweka sawa mambo haya,
Clouds wataitisha mkutano mkubwa wa waandishi wa habari ili kuifahamisha
jamii ni nini hasa kinaendelea.
Baada ya bosi huyo kutoa ufafanuzi
juu ya tuhuma za msanii huyo, Ijumaa lilimtafuta meneja wake Jide,
Gardner G. Habash ili aweke wazi kama tuhuma alizotoa mwanamuziki huyo
zina ushahidi wa kushika, lakini bila mafanikio.
JIDE KATIKA SIKU ZA KARIBUNI
Katika siku za hivi karibuni, Jide
amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kueleza jinsi anavyoandamwa na
kituo hicho cha redio na kusababisha kuibuka kwa mijadala mbalimbali
kutoka kwa wasomaji wake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment