WATU wanaodhaniwa
kuwa ni vibaka kutoka katika machimbo ya dhahabu ya Nyangarata na Mwime
wilayani Kahama mkoani Shinyanga,ambayo yamekwisha uzalishaji
wake,wamemuua
askari wa Usalama barabarani;Salum Mtepa mwenye cheo cha Staff
Sajenti,kwa
kumpiga na kitu kizito kifuani.
Tukio hilo limetokea
nyumbani kwake eneo la Majengo mjini Kahama usiku wa kuamkia leo baada
ya watu
hao wanaokadiriwa kuwa wanne kufika nyumbani kwake na kuvunja kibanda
cha
biashara kwa lengo la kuiba ndipo askari huyo alipotoka nje kwenda
kupambana
nao.
Kwa mujibu wa taarifa
ya Mkuu wa Polisi wilaya ya Kahama George Simba,askari huyo alipigwa na
kifaa
hicho kifuani wakati akijaribu kupambana na vibaka hao,hali iliyopelekea
kuvuja
damu nyingi ndani ya kifua na kusababisha kifo chake.
Simba amesema hali ya
vibaka katika mji wa Kahama ni mbaya kwani wameongezeka kutokana na
machimbo ya
Nyangarata kujaa maji na Mwime kuisha uzalishaji wake,hali iliyofanya
vijana
wengi kutoka kwenye maeneo hayo bila kuwa na fedha.
Amesema hivi sasa
wimbi la vibaka hao limekuwa tishio huku akiahidi kupambana nao ikiwa ni
pamoja
na kuwasaka kwa nguvu zote vibaka waliohusika na kifo cha askari huyo wa
usalama barabarani,ingawa hadi jana hakuna mtu yeyote aliyekuwa
amekamatwa juu
ya kuhusika na tukio hilo.
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment