Pamoja na kupanda kwa gharama za
maisha ikiwamo manunuzi ya vyakula, Serikali imesema itaendelea kutumia
gharama ya Sh1,500 kwa wanafunzi wa bweni kwa shule za msingi nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Agrey Mwanri kuwa Serikali
inatambua gharama za maisha zimepanda lakini haina namna kuhusu
kupandisha viwango hivyo.
"Ni kweli bei za vyakula katika masoko
makubwa pamoja na mambo mengine mengi zimepanda, kwa sasa Serikali
haina uwezo wa kutamka kuhusu kupandisha kiwango hicho kama alivyoomba
mbunge, hivyo tutaendelea na kiwango cha Sh1,500 kwa siku kwa mwanafunzi
wa shule ya msingi wa bweni," alisisitiza Mwanri.
Mbunge wa Longido ataka wanafunzi
wapandishiwe gharama Katika swali la msingi Mbunge wa Longido, Michael
Laizer (CCM) alihoji ni kwa nini Serikali inaendelea kutumia kiwango cha
Sh1, 500 kwa wanafunzi ambacho kimepitwa na wakati.
Mbunge huyo alitaka Serikali ipandishe
kiwango cha gharama hizo na kufikia Sh2,500 kwa siku ili kuendana na
wakati ulipo kwa sasa.
Kwa mujibu wa Laizer, hata kiwango
kilichoelezwa na Serikali cha Sh1, 500 bado kuna wazabuni wengi ambao
wanaidai Serikali kiwango kikubwa cha fedha.
Kuhusu wazabuni, Naibu Waziri aliahidi
kuwa Serikali iko katika mchakato wa kumaliza madeni hayo mapema
iwezekanavyo ili waendelee kutoa huduma nzuri kwa wanafunzi.CHANZO
MWANANCHI
Post a Comment
toa maoni yako hapa pia usisahau kuweka coment